2015-12-04 15:38:00

Mchakato wa amani ya kudumu eneo la Mindanao wajadiliwa na Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 4 Desemba 2015 amekutana na kuzungumza na Rais Benigno S. Aquino III wa Ufilippini ambaye baadaye amekutana pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo yao, viongozi hawa wawili wamejikita katika majadiliano ya kina katika makundi mbali mbali ya kijamii nchini Ufilippini pamoja na mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi na maendeleo ya wengi. Kwa namna ya pekee, wamegusia mchakato wa amani huko Mindanao kwa kuonesha matumaini kwamba pande zote zinazohusika, zitajitahidi kuhakikisha kwamba amani ya kweli na ya kudumu inapatikana katika Ukanda huu. Wakati wa mazungumzo haya, wamebadilishana pia mawazo kuhusiana na masuala ya kimataifa na kikanda kwa kufanya rejea kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi sanjari na mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi COP21 unaoendelea mjini Paris, Ufaransa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.