2015-12-04 06:54:00

Biblia ni moto wa kuotea mbali!


Biblia ni kitabu kitakatifu, moto wa kuotea mbali, sababu na chanzo cha mateso na dhuluma dhidi ya baadhi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia; mwaliko ni kuisoma, kuitafakari na kuwashirikisha wengine bila kuwa na makunyanzi, kwani kwa kufanya hivi, mwamini anaweza kukutana na Yesu Kristo katika maisha yake. Kwa ufupi hivi ndivyo anavyoandika Baba Mtakatifu Francisko katika utangulizi wa Biblia ya Vijana, iliyofanyiwa tafakari na vijana wenyewe na kuchapishwa kwa lugha ya Kijerumani. Huu ni mradi ambao umewashirikisha wataalam wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu na kwamba, utangulizi wa Biblia hii kwa lugha ya Kiitalia umechapishwa kwenye Jarida la Civiltà Cattolica.

Baba Mtakatifu anawaambia vijana kwamba, hawataweza kuamini macho yao wakiona Biblia yake ambayo amekuwa akiitumia kwa zaidi ya miaka hamsini, imezeeka na kudumaa. Pengine baadhi yao wangeweza kumwonea huruma na kumnunulia Biblia mpya kwa bei cheee kabisa! Lakini anasema hataki, kwani ya kale ni dhahabu. Anaipenda Biblia yake kwa moyo na akili zake zakezote. Ni Biblia ambayo imeona furaha ya moyo wake, ikalowa kwa machozi ya uchungu na majonzi, kwa hakika anasema Baba Mtakatifu "hii ndiyo hazina yangu na kamwe siwezi kuiachia".

Huu ni ushuhuda unaobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wa Baba Mtakatifu kwa vijana wa kizazi kipya ili kuwahamasisha kupenda kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao! Anawahamasisha vijana kuendelea kusoma Biblia na kamwe wasiitundike kwenye shelfu za vitabu kwani siku moja watashangaa kuona watoto wao wameipeleka kwa wauza mitumba! Tangu mwanzo wa Kanisa, Wakristo wameteseka na kudhulumiwa kwa vile walikuwa wanatoa ushuhuda wa maisha yao ya Kikristo kwa kuvaa Msalaba au hata pengine kwa kukutwa na Biblia.

Kuna baadhi ya watu wanaiona Biblia kuwa ni kitabu cha hatari kabisa katika usalama wa utawala wao, kumbe, kwa Mkristo anayekamatwa na Biblia anashughulikiwa kama gaidi anayetembea na bomu mikononi mwake! Mahtma Gandhi aliwahi kusema kwamba, Wakristo wanamiliki kitabu ambacho kinaweza kuleta mageuzi makubwa katika tamaduni za watu kwa kujikita katika amani, lakini kwa bahati mbaya wengi wao wanaiona Biblia kuwa ni kazi nzuri ya fasihi simulizi. Baba Mtakatifu anauliza swali la msingi, ikiwa kama mambo ni hivi mbona kuna wakristo wanateseka na kunyanyasika kwa sababu ya Biblia?

Anakumbusha kwamba, Biblia ni kielelezo cha nuru ambayo imekuja ulimwenguni na kamwe haitweza kuzimishwa! Biblia imeandikwa si kwa ajili ya kuhifadhiwa kwenye shelfu za vitabu, bali kuwa mikononi mwa waamini ili waweze kuisoma na kuitafakari, tayari kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Vijana wanahimizwa na Baba Mtakatifu kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuwa na Biblia kila mahali wanapokwenda, wawe tayari kujisomea na kuwashirikisha pia rafiki zao, kwani mambo mazuri wanapaswa kushirikishwa wengine pia.

Vijana wajitahidi kusoma Biblia kwa umakini mkubwa na wala wasiridhike kuisoma juu juu pasi na kuzama kwa undani zaidi ili kung’amua kile ambacho Mwenyezi Mungu anakitaka kwa vijana kutoka katika undani wa mioyo yao! Kwa njia hii, Neno la Mungu  litakuwa kweli ni cheche za mabadiliko katika maisha. Baba Mtakatifu anawaambia vijana wa kizazi kipya kwamba, Yeye anajisomea Biblia kwa kuchukua sehemu ya Neno la Mungu na baadaye kuifanyia tafakari ili iweze kuzama zaidi katika akili na moyo wake, ili kumpatia nafasi Yesu aweze kumwangalia kwa jicho la upole na upendo.

Wakati mwingine Yesu hasemi neno lolote, hapo huwa anajisikia kuwa mkavu katika maisha yake ya kiroho, lakini anaendelea kumsubiri akitafakari na kusali. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, anapenda kusali akiwa amekaa kwani akipiga magoti anaumia sana, wakati mwingine anajikuta amekwisha zama usingizini, yote hii ni sehemu ya maisha. Baba Mtakatifu anawaambia vijana ikiwa kweli wanataka kumfurahisha katika maisha, basi wachangamkie kusoma Biblia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.