2015-12-04 11:38:00

Barua ya kichungaji kutoka kwa Askofu mkuu Ruwa'ichi Jimbo kuu la Mwanza


Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Mwanza ameandika Barua ya kichungaji kwa Familia ya Mungu Jimboni humo akigusia kwa namna ya pekee kuhusu: Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, Mwaka wa Wanaume Wakatoliki Jimbo kuu la Mwanza; Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu; Makongamano ya Utoto Mtakatifu na Ekaristi Takatifu ngazi ya Kitaifa; Mikakati ya ujenzi wa Kanisa kuu; Maisha ya kiroho na Sakramenti za Kanisa; Mipango ya kichungaji na kiuchumi, Jimbo kuu la Mwanza, mwishoni ni salam na matashi mema kwa ajili ya maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli na Mwaka mpya 2016. Sasa unaweza kuendelea kwa raha zako mwenyewe!

Ninawatakia neema na baraka za Bwana wetu  Yesu Kristo – Mfalme.

Tukiwa tunaendelea na majukumu yetu kama wafuasi na mashahidi wa Bwana wetu Yesu Kristo, ninafurahi kuwaandikia barua hii ya kichungaji kwa lengo la kuwafahamisha kuhusu maswala mbalimbali ya kichungaji yanayotuhusu sote kwa pamoja kama familia ya Mungu ya Jimbo Kuu la Mwanza.Ninawasihi wanakanisa wote, na kwa namna ya pekee wale wote walioaminishwa majukumu katika kanisa, kama vile mapadre, mashemasi, makatekista, wajumbe wa kamati tendaji za parokia, halmashauri ya walei, viongozi wa vyama vya kitume na waratibu wa makundi ya wanavuguvugu wa imani – kuhakikisha kwamba ujumbe huu unawafikia walengwa wote. 

Barua hii ya kichungaji inabainisha baadhi ya mambo muhimu yatakayojitokeza kwa namna ya pekee katika kalenda yetu tutakapokuwa tukiishi imani na utume wetu katika mtiririko wa mwaka wa Kanisa. Bila shaka hatujidai kuyagusia yote. Kwa kuzingatia uzito wa maswala yatakayoainishwa katika barua hii, ninawaalika wote kufanya juhudi za makusudi ili mambo yanayobainishwa  yanazingatiwe na kufanyiwa kazi kwa uzito na umakini unaotakiwa kwa lengo la kumtolea Mungu sifa na pia kuwajenga na kuwatakatifuza wanadamu.

Yafuatayo ni maswala husika:

MWAKA WA WATAWA:

Ninapenda kuwakumbusha waamini wote na kwa namna ya pekee watawa\watu wa maisha ya wakfu kwamba tunaendelea na maadhimisho ya Mwaka wa Watawa uliowekwa kwa ajili ya kanisa lote. Tunaelekea kwenye hitimisho la adhimisho hilo muhimu.Ninawapongeza watawa kwa jinsi walivyojituma kutumia vema fursa hiyo muhimu ya kujitathmini, kujipanga na kujiimarisha katika ufuasi, uwakfu na utume wao.

Ninawashukuru mapadre na waamini walei waliolipa uzito swala la Mwaka wa watawa na kuungana nao kwa ukunjufu na ukarimu katika kuadhimisha tukio hilo la neema na baraka kwa watawa na kwa kanisa lote. Katika Jimbo kuu la Mwanza, adhimisho la Kilele cha Mwaka wa Watawa kitafanyika hapa Kawekamo mwezi  Februari kwa utaratibu ufuatao: Mkesha wa Hitimisho la Mwaka wa Watawa: Huu utafanyika jioni ya tarehe 6 Februari 2016. Kutakuwa na fursa ya maungamo, mada, kuabudu na mengineyo kama yatakavyopangwa na viongozi wa Umoja wa Watawa Jimboni. Misa ya Hitimisho la Mwaka wa Watawa: Tutaadhimisha Misa ya kuhitimishwa Mwaka wa Watawa tarehe 7 Februari 2016 katika Madhabahu ya Kawekamo. Hili ni adhimisho linalohusu kanisa lote. Kwa hiyo, wawakilishi kutoka parokia zote wafike kuonyesha mshikamano na watawa na pia kutoa shukrani kwa Mungu kwa zawadi ya watawa.

MWAKA WA WANAUME WAKATOLIKI:

Imepita miezi saba tangu tulipozindua rasmi mwaka wa wanaume wakatoliki Jimbo Kuu la Mwanza. Ikumbukwe kwamba wahusika wa adhimisho hilo ni wanaume wote:Waliobatizwa; Wenye umri wa miaka 18 na kuendelea. Ninapenda kutoa shukrani za pongezi kwa mapadre, makatekista, viongozi wa halmashauri ya walei na wana UWAKA wote ambao wamejituma kwa dhati katika kuhamasisha na kufanikisha maadhimisho ya Mwaka wa Wanaume Wakatoliki.

Aidha ninawapongeza sana wanaume wakatoliki wote ambao wametambua umaana na kujituma kushiriki katika kutekeleza maudhui ya mwaka wao maalum. Tutambue kwamba muda uliobaki si mwingi. Ninawahimiza wanakanisa wote na kina baba kwa namna ya pekee kutumia vema zaidi muda uliobaki hasa kwa: Kuonyesha mwamko mpya wa imani na ushuhuda. Kuadhimisha kwa ukunjufu tunu na fursa walizojaliwa na Mungu: kama vile ubaba (ambao kwa asili ni wasifu wa Mungu) ambao sisi tunashirikishwa; uongozi (kichwa cha familia, yaani kanisa la nyumbani); malezi ya kiutu, kiimani na kimaadili; upatanishi; ulinzi wa uhai, usalama na amani; watetezi wa haki; kielelezo cha kujituma na kuwajibika; kielelezo cha kujiamini; mhimili wa uongozi na kurithisha imani.

Kutambua kwamba kina baba ni hazina na nguvu kubwa ya ajabu. Kwa sababu hiyo, uwepo na ushiriki wa dhati wa kinababa katika maswala ya familia, jumuia na kanisa ni chimbuko la nguvu, usitawi, faraja na fanaka. Tukizingatia ukweli huu wa msingi, tutafanya bidii zaidi katika kuenzi na kufaidi hazina inayowakilishwa na wanaume wakatoliki. Ninawaalika kina baba wenyewe kwa upande mmoja, na wachungaji kwa upande wa pili kufanya tathmini ili kuona tumefanikiwa kiasi gani na yapi yanayotudai kuyafanyia kazi ili yapatikane mafanikio zaidi. Napenda kuhitimisha kwa kutamka kwamba tunanuia kufanya tathmini kwa ngazi ya ofisi na kupanga tarehe ya kuadhimisha kilele cha mwaka wa wanaume wakatoliki. Uamuzi juu ya tarehe ya adhimisho la kilele cha Mwaka wa wanaume wakatoliki mtatangaziwa katika barua zijazo.

MWAKA WA HURUMA YA MUNGU:

Tarehe 13 Machi 2015, alipokuwa akiadhimisha mwaka wa pili wa kuchaguliwa kwake kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko alitangaza azma yake ya kuadhimisha Jubilei Maalum ya Huruma ya Mungu. Amefanya hivyo akisukumwa na mwono na uelewa sahihi wa kichungaji. Hatimaye, tarehe 11 Aprili 2015, Baba Mtakatifu alitoa hati rasmi inayojulikana kwa jina la “Misericordiae vultus”, yaani “USO WA HURUMA”. Katika hati hiyo, Baba Mtakatifu Francisko anatupatia ufafanuzi wa kiteolojia wa dhana ya huruma. Zaidi ya hayo, anatoa mtiririko mzima wa jinsi Mwaka wa Jubilei ya Huruma unavyopaswa kuadhimishwa.

Ninamwalika kila mmoja na wote kwa pamoja kulipokea tangazo hilo kwa moyo mkunjufu na wa shukrani. Aidha ninamwalika kila mwanakanisa na mtu yeyote mwenye mapenzi mema, kujipanga vema ili ashiriki vizuri na kufaidika na maadhimisho yanayohusu Mwaka wa Huruma ya Mungu. Ili kufanikisha uelewa na ushiriki wa adhimisho la Mwaka wa Huruma ya Mungu, ninaaagiza kwamba: Kila padre, shemasi, katekista na kiongozi wa halmashauri ya walei, asome kwa makini kijitabu cha “Uso wa Huruma”, ili aweze kuwasaidia wanakanisa wengine ipasavyo.

Kila Jumuiya ndogo-ndogo ya Kikristo ijipatie nakala za kijitabu cha Uso wa Huruma na kukisoma hatua kwa hatua katika mtiririko wa Mwaka wa Huruma. Aidha, kila wanapokusanyika, wanajumuia wasali Sala maalum aliyoitunga Papa Francisko kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Wajipange pia kujipatia fursa ya kusali Rozari ya Huruma ya Mungu na Novena ya Huruma ya Mungu. Mahubiri na katekesi sahihi na ya kina viandaliwe ili  kuwasaidia wanakanisa kusameheana na kupatana, kupokea huruma ya Mungu tunayozawadiwa bure, kutekeleza matendo ya huruma kwa furaha na ukunjufu (kwa wagonjwa, wadhambi, waregevu wa imani, maskini, wafungwa, wapweke, wanaoonewa na kusetwa n.k.), kuielewa na kuiishi sala ya Bwana – “Baba Yetu” – hasa kile kifungu kisemacho: “Utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi wale waliotukosea!!!”.

Wakristo wafundishwe kujichunguza nafsi na kisha, wakisukumwa na toba ya kweli, wakimbilie kwenye kiti cha Huruma ya Mungu, yaani cha Kitubio ili kuungama, kushauriwa na kupatanishwa na Mungu, pia na wenzao, nafsi zao na mazingira wanamoishi. Mapadre waweke kipaumbele zaidi katika utume wa kuwaganga na kuwatibu waamini kwa kuadhimisha vema zaidi, kwa ukarimu, huruma na upendo wa kichungaji – Sakramenti ya upatanisho au kitubio. Katika mwaka wote wa Huruma ya Mungu, Mapadre wanaruhusiwa kuondolea dhambi zilizozuiliwa. Wafanye hivyo kwa unyofu, ukomavu wa kichungaji, huruma na hofu ya Mungu. Katika Mwaka wa Huruma ya Mungu, Picha maalum ya Yesu chimbuko la itazungushwa katika Parokia zote za Jimbo Kuu la Mwanza. Zoezi hilo lifanyike kwa heshima, uangalifu na uchaji wa hali ya Juu. Mafundisho bayana yatolewe kuhusu uhusiano kati ya Mateso, Kifo na Ufufuko wa Bwana Wetu Yesu Kristo na swala la Huruma ya Mungu.

Bila shaka, katika hija ya Picha ya Huruma ya Mungu katika maeneo ya parokia, jumuia, na familia, waamini na watu wenye mapenzi mema, zitakuwepo fursa kwa  waamini na watu wenye mapenzi mema kutoa matoleo na sadaka zao kwa kadiri watakavyoguswa. Ninaagiza kwamba matoleo hayo yapokelewe kwa shukrani, heshima, uaminifu na uchaji. Aidha nusu ya matoleo hayo yatumike katika Parokia husika na nusu iwasilishwe katika ofisi za jimbo kwa kusaidia utume wa kijimbo.

Wakati wote wa mwaka wa Huruma ya Mungu, waamini wasali binafsi, kifamilia, kijumuia na hata katika mikusanyiko mingine sala maalum iliyotungwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa lengo hilo. Ifuatayo ni tafsiri ya sala hiyo:

“Ee Bwana Yesu Kristu, umetufundisha na kutuagiza tuwe na huruma kama Baba wa mbinguni alivyo na huruma. Pia, umetufundisha kwamba anayekuona wewe, amemwona Baba! Tuonyeshe uso wako, nasi tutaokokolewa! Mtazamo wako wa huruma ulimnasua Zakayo na Matayo kutokana na utumwa wa fedha; yule mwanamke mzinzi na Maria Magdalena kutokana na utumwa wa kutafuta raha kutoka kwa viumbe, na pia mtazamo huo wa huruma ulimchoma Petro hata akalia kwa majuto baada ya kukukana; na tena, mtazamo huo wa huruma ulimhakikishia paradiso, yule mwizi aliyetubu. Tujalie kufarijiwa na yale maneno uliyomtamkia yule mwanamke msamaria ulipomwambia: ‘kama tu ungaliitambua zawadi ya Mungu!’

Ee Bwana Yesu, wewe ni uso unaoonekana wa Mungu asiyeonekana, Mungu anayedhihirisha uwezo wake hasa kwa njia ya huruma na msamaha. Lijalie kanisa lako lipate kudhihirika zaidi kuwa ni uso wako unaoonekana katika ulimwengu unaohitaji kukutambua kama Mfufuka na Mtukufu. Wewe uliridhia kujiteulia mawakili, wahudumu wa kanisa walio wadhaifu, ili waweze kusukumwa kuwahurumia wale wanaosakamwa na ujinga na makosa. Jalia kwamba yeyote anayewaendea hao mawakili wako, ahisi kuwa anatafutwa, kupendwa na kusamehewa na Mungu.

Tunakusihi umpeleke Roho wako Mtakatifu na umweke wakfu kila mmoja wetu kwa mpako wa Roho huyo, ili jubilei hii ya Huruma iwe kwetu mwaka wa neema itokayo kwa Bwana. Nalo kanisa lako, likijawa mwamko mpya, liwapelekee maskini habari njema, litangaze uhuru kwa wafungwa na walioonewa na kuwarudishia vipofu uwezo wa kuona tena. Haya tunakuomba Ee Bwana Yesu, kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Huruma.  Unayeishi na kutawala pamoja na Baba na Roho Mtakatifu, milele na milele – amina.”

Napenda kuwafahamisha pia kwamba ofisi ya Baba Mtakatifu imetoa wimbo rasmi wa kusindikiza maadhimisho ya Jubilei ya Huruma ya Mungu. Ifuatayo ni tafsiri ya wimbo huo: Kiitikio: Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma. 

Mshukuruni Mungu kwa kuwa ni Mwema, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Ameiumba nchi kwa hekima, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Anawaongoza watu wake katika mapito ya historia, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Anawasamehe na kuwakaribisha watoto wake, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. – Kiitikio.

Mshukuruni Mwana wa Mungu, Mwanga wa mataifa. Kwa maana fadhili zake zadumu milele.  Ametupenda kwa ‘moyo wa nyama’ Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Kama tunavyotunukiwa naye, nasi pia tumrudishie, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Mioyo radhi kwa wote wenye njaa na kiu, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. – Kiitikio.

Tumsihi Roho atumiminie vipaji vyake saba, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Chimbuko la wema wote na faraja tamu kabisa, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Kama tunaofarijiwa naye, sisi nasi tuwafariji wenzetu, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Upendo huvumilia yote, hustahimili yote, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. – Kiitikio.

Tumwombe Mungu, asili ya amani yote, atujalie amani, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Dunia ina kiu ya Habari Njema ya Ufalme, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Furaha na msamaha mioyoni mwao walio wanyofu, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. Mbingu na dunia vitafanywa upya, Kwa maana fadhili zake zadumu milele. – Kiitikio. Ninawaalika wataalam wa muziki kuandaa tungo za kufaa, ili tuwe na nyimbo nzuri zinazotokana na mashairi hayo hapo juu. Uzinduzi wa Mwaka wa Huruma ya Mungu Utafanyika kama ifuatavyo: Mkesha wa Uzinduzi: tarehe 8 Desemba 2015 katika Madhabahu ya Kawekamo. Jioni hiyo, kutakuwa na maungamo, mada mahususi, kuabudu Ekaristi takatifu, filamu ihusuyo huruma na upatanisho. Misa Kuu ya Uzinduzi wa Mwaka wa Huruma ya Mungu itafanyika katika Madhabahu ya Kawekamo tarehe 9 Desemba 2015. Wahusika wanaopaswa kushiriki ni mapadri, watawa na waamini walei kutoka Parokia zote na asasi za kikanisa.

MAKONGAMANO YA KITAIFA: LA EKARISTI  &  UTOTO MTAKATIFU:

Mwaka 2016 , kutakuwa na adhimisho la Kongamano la Ekaristi takatifu kimataifa. Kongamano hilo litafanyika mwezi Januari nchini Ufilipini, katika Jimbo kuu la Cebu. Kwa wengi wetu, huko ni mbali kulingana na uwezo wetu. Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), limejiwekea utaratibu wa kuadhimisha makongamano ya Ekaristi Kitaifa. Hilo linalenga kuwapatia waamini fursa ya kutafsiri katika mazingira ya Kitanzania, yale ambayo wanakanisa wenzao wanayapata katika kushiriki kwao katika Kongamano la Ekaristi la Kimataifa.

Kongamano lililopita la kitaifa la Ekaristi lilifanyika huko mjini Iringa mwaka 2012. Kongamano hilo liliwashirikisha wanakaanisa kutoka majimbo yote ya Tanzania. Aidha, kongamano hilo lilikuwa ni fursa ya: Kutoa ushuhuda wa hadhara wa imani yetu. Kuimarika na kuimarishana katika imani, maadili na utume. Kuamshwa kimaadili. Kupata katekesi kuhusu maana na nafasi ya Ekaristi takatifu katika maisha ya mkristu binafsi na yale ya Kanisa. Kuamsha roho na moyo wa kimisionari. Kuwagusa na kuwavuta wengine kumfahamu, kumwamini, kumpenda na kumwabudu Yesu wa Ekaristi. Kuoanisha imani na maisha kwa jinsi isiyoruhusu mpasuko. Kuzingatia wito wa msingi wa kila Mkristu, yaani kuwa watakatifu. 

Ninafurahi kuwatangazieni rasmi kwamba Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), limeamua kwamba kongamano lijalo la Ekaristi la kitaifa lifanyike hapa kwetu Mwanza, hasa katika Madhabahu ya Kawekamo. Hii ni heshima kubwa. Hii ni fursa mahususi ya kuimarisha imani, ushuhuda na utume wetu. Ninamwalika kila mwanajimbo kuu la Mwanza atambue kwamba tumepewa hadhi ya kuwa wenyeji na washiriki wa mstari wa mbele wa tukio hilo takatifu. Heshima hiyo ina gharama zake. Ninawaomba wanajimbo wote: walei, watawa na mapadre, tuwe wenyeji wazuri na washiriki bora na makini wa tukio hilo la neema.

Ratiba mahususi ya Kongamano lenyewe tutapewa baadaye. Hata hivyo, mpangilio mpana wa kongamano ni kama ifuatavyo:

Ninachukua fursa hii kuwasihi wanajimbo kulipokea kongamano hilo kwa moyo radhi na kujipanga kushiriki katika harakati za kulifanikisha kongamano kwa sala, hali na mali. Ninawaomba wakuu wa asasi za Kanisa, hasa mashule wajitahidi kuweka mpangilio utakaoruhusu shule kufungwa mapema, kabla ya tukio ili kufanikisha ugeni mkubwa utakaotukabili. Aidha, ninawasihi wanakanisa wenye nafasi za kupokea wageni, wawe radhi kukaribisha wageni katika nyumba zao; nao wenye nyumba za wageni kama vile mahoteli na hosteli, wawe radhi kuwapokea wageni kwa gharama zinazobebeka. Natanguliza shukrani na matashi mema ya neema na baraka kwa wote watakaojitokeza kwa kutoa ushirikiano.

Tumeunda kamati ratibishi ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Padre Valentini Kabati, Makamu wa Askofu. Kamati hiyo inafanya kazi bega kwa bega na kamati ya kitaifa kupitia ofisi ya kichungaji ya TEC. Tafadhali yapokeeni na kuyazingatia maelezo na maelekezo ambayo mtapelekewa na kamati hiyo. Ikumbukwe kwamba, muda uliobaki ni mchache. Kwa hiyo, tuutumie vizuri na kwa umakini mkubwa katika kujiandaa. Sambamba na Kongamano la Ekaristi Kitaifa, litafanyika pia Kongamano la Utoto Mtakatifu Kitaifa. Sisi wana-Mwanza na watoto wetu, ni wenyeji wa kongamano hilo. Ninawasihi wazazi na wanakanisa wote kujipanga kuwawezesha watoto wetu:

Wakati wa hitimisho la sherehe za Shukrani na Ukarimu mwaka huu, wanajimbo wote tulikabidhiwa Mpango Mkakati wa ujenzi wa Katedrali, yaani kanisa kuu la Jimbo. Ninachukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wale wote ambao wamejipanga kwa moyo radhi na ukarimu katika: Kuufikisha mchakato huo kwa wadau wengi katika parokia na asasi za kikanisa za Jimbo Kuu la Mwanza. Wale walioainisha mipango mahususi ya kutekeleza mchakato wenyewe hasa kwa kuzingatia kipengele cha kwanza na cha pili cha namna za kutafuta michango.

Kwa upande mwingine, ninasikitika kwamba katika baadhi ya maeneo, ni kama vile mpango wote umeswekwa mvunguni, kwani katika maeneo hayo, hakuna kinachoendelea. Wahusika wanajua wanachokifanya! Napenda kuwaalika wajitume kwa ukunjufu na uwajibikaji zaidi! Ninawasihi waitambue shughuli nzima kama ni yao, inawahusu na inawadai! Ninachukua nafasi hii, kuagiza kwamba katika kila Parokia, zifanywe juhudi za wazi na makusudi – kuunda kamati itakayoratibu uhamasishaji wa ujenzi wa Katedrali. Ninatambua kwamba baadhi ya parokia tayari zina kamati hiyo. Zile ambazo hazina bado, zifanye bidii kuunda na kuweka mikakati ya kuiwezesha kufanya kazi kwa malengo na ufanisi.

Kufuatia ombi na pendekezo la kamati nimewateua mapadre watatu ili wahusike na uratibu wa maswala ya ujenzi wa Kanisa kuu. Mapadre hao ni: Fr. Alex Kitwala, Fr. Fidelis Munga na Fr. Onesimo Shingelwa. Mapadri hawa wamekabidhiwa jukumu na mamlaka ya kufanya kazi bega kwa bega wakishirikiana na ile Kamati Kuu ya Ujenzi wa Kanisa kuu. Wao na wanakamati, watajipangia taratibu za kutembelea Maparokia ili kuufafanua mpango mkakati, kuhamasisha ushiriki wa wabatizwa na shughuli nyingine zinazohusiana na jukumu hili kubwa linalotukabili. Ninawasihi na kuwaagiza wanakanisa wote kuwapa ushirikiano wa dhati. Nachukua fursa hii kuwakumbusha wanajimbo yote kwamba kuna wingi wa neema na baraka katika umoja na ukarimu hasa katika yale yamhusuyo Mungu na watu wake!

SAKRAMENTI ZA KANISA

Nyakati zetu hizi, zinagubikwa changamoto nyingi na nzito kuhusu imani. Ukweli huo unatudai tujizatiti visuri zaidi ili kuilinda imani yetu isivurugwe, kudhoofishwa wala kupotoshwa. Kwa hiyo, kufuatia tafakari ya kina, tumeona kwamba upo ulazima wa kuimarisha misingi ya imani hasa kwa kutazama upya malezi na maandalizi wanayopata wale wanaojiandaa kupokea sakramenti mbalimbali. Kwa hiyo, ninachukua fursa hii kutoa maelekezo wa jumla hasa kuhusu sakramenti zifuatazo:

1.UBATIZO:

Sakramenti ya ubatizo inapotolewa kwa watoto wa shule au watu wazima, ihakikishwe kwamba wahusika wanapewa mafundisho ya msingi ambayo mtiririko wake haupaswi kupungua miaka miwili. Mafundisho hayo yaandaliwe vizuri na yasindikizwe na maadhimisho ya hatua muhimu za safari ya mkatekumeni. Mapadre wafuatilie kwa karibu na kujiridhisha kwamba mwendo wa mafundisho ni sahihi na wa kuridhisha, ili wakatekumeni wapatiwe msingi imara kwa ajili ya maisha, imani, ufuasi na utume utakaowapasa kama wakristo. Kwa upande wa ubatizo wa watoto wachanga, wazazi na wasimamizi wapewe katekesi ya kufaa ili kuwawezesha kutekeleza vema jukumu la kumlea mtoto kiutu na kikristo akishabatizwa. Ihakikishwe kwamba ubatizo hautolewi kwa mazoea tu, bali kwa uelewa na uwajibikaji.

2.EKARISTI:

Siku hizi, kuna uelewa mdogo na wa kutisha kuhusu maana, utakatifu, heshima na jinsi ya kujiweka mbele ya Ekaristi takatifu. Ukosefu huo wa uelewa unazaa purukushani na hata vitendo vya kukufuru na kuchezea matakatifu. Hii ni changamoto kubwa. Jambo hili linapaswa kumkera kila mkristu mwelewa na mwenye staha. Ili kuondoa kero hii, ninaagiza kwamba wale wote wanaojiandaa kwa komunio ya kwanza wao pia wapewe mafundisho yasiyopungua miaka miwili. Hayo pia yaandaliwe kwa uangalifu, ueledi na kina. Watoto wa shule wakiandaliwa ipasavyo, wakishakupimwa na kuonyesha uelewa wa kuridhisha, waruhusiwe kupokea komunio ya kwanza wakiwa walau darasa la tatu.

3.KIPAIMARA:

Hii ni Sakramenti ya ukomavu wa Kikristo. Waamini wakishaimarishwa, wanatarajiwa wajidhihirisha kuwa walinzi wa imani yao, washirikishi wa imani kwa njia ya ushuhuda wa maisha na maneno yao, manabii wa kweli, yaani wajumbe wake Mungu walio tayari kuusimamia ukweli na kuyatakatifuza malimwengu na jamii kwa ujumla kwa njia ya maisha na utume wao. Siku hizi, baadhi ya watoto wanaruhusiwa kupokea kipaimara wakiwa wadogo sana na pengine wenye uelewa mdogo sana wa imani yao. Jambo hili lina hatari zake. Busara, ueledi wa kichungaji na uwajibikaji visipozingatiwa, utakuta kwamba watoto wa namna hiyo, wakishaimarishwa katika umri mdogo, hawapati tena fursa ya mafundisho na malezi ya imani labda mpaka watakapofika kuandikisha ndoa. Ukweli huu unapaswa kutuhangaisha na kutufikirisha.

Ili kuhakikisha kwamba waimarishwa wanasindikizwa kwa mafundisho ya kutosha, ninaagiza kwamba kuanzia mwaka ujao, wale wote wanaojiandaa kwa sakramenti ya kipaimara, wao pia wapate katekesi, yaani mafundisho ya imani yasiyopungua miaka miwili. Kwa mantiki hiyo, mathalan watoto wa shule ya msingi wakishapimwa kuhusu uelewa na ukomavu wao kiimani na kimaadili, waruhusiwe kupewa kipaimara wakiwa darasa la tano au la sita. Baada ya kupata sakramenti, ifanywe mipango ya dhati ya kuwapatia “mistagogia”, yaani Katekesi endelevu yenye lengo la kuwasimika zaidi katika imani yao.

4.KITUBIO:

Katika nyakati zetu, ipo hatari kubwa ya dhamiri kulemaa na hata kufa. Katika hali hiyo, watu wanaelekea kutokuwa na hisia kuhusu dhambi. Ndiyo maana wako watu ambao hawaungami tena. Ninaliona hilo kama hali ya kuwa butu kiroho. Ubutu huo unatufanya kuwa watumwa wa giza na wahanga wa kifo cha kiroho. Bila shaka, uelewa finyu wa imani, udhaifu katika mazoea ya kulisoma na kulitafakari Neno la Mungu, kuchanganyikana na watu wa imani nyingine na kuathiriwa nazo, kukosa katekesi mahususi na pia kukosa ukaribu wa kichungaji kunachangia kulikuza tatizo.

Kwa hiyo, ninawahimiza mapadre wajitahidi zaidi kulea dhamiri kwa njia ya mahubiri ya kina, katekesi, utume wa Biblia, ukaribu na usikivu wa kichungaji ili kuwasaidia na kuwanusuru waamini. Aidha wajipe nafasi zaidi kwa ajili ya kuwaganga waamini kiroho. Nao waamini, wajijali na kujitunza kiroho kwa kutafuta mara kwa mara, fursa ya kitubio. Bila shaka, ni muhimu mkristu akatafuta fursa ya kuungama kila anapojitambua kuwa ameanguka katika dhambi. Hata hivyo, nishauri kwamba walau kila mwezi, mkristu ajitafiti moyo na kuikimbilia kiti cha huruma ya Mungu ili kuungama na kupata maondoleo. Niwatie wote moyo kwa kukumbusha kwamba tunao wajibu wa kujijali na kujitunza kiroho kama vile tunavyofanya kuhusu miili yetu kwa kushughulikia usafi na tija yake. Mkristu wa kweli hapaswi kuogopa kujitafiti kwa unyofu na kuungama. Mkristu wa kweli asikubali kung’ang’ana na dhambi. Yesu ametuweka huru, basi tupende kuwa huru.

5.NDOA:

Sakramenti takatifu ya ndoa ni ya msingi kabisa katika Kanisa. Sakramenti hii inahusiana na wito, uwakfu na utume wa mkristo mlei. Wengi katika kanisa wamepewa wito huu. Wito wa ndoa unamdai mhusika kuzingatia upendo, umoja, uaminifu na udumifu kwa maagano yanayowekwa mbele ya Mungu, mwenzi wa ndoa na kanisa. Uwakfu wa ndoa unatokana na ukweli kwamba yenyewe ni kifungo kitakatifu kati ya mume mmoja na mke mmoja, kifungo alichokianzisha na kukibariki Mungu mwenyewe.

Utume wa ndoa unamdai mwanandoa kuliunda na kulijenga kanisa la nyumbani yaani familia. Wanandoa wanatekeleza hilo kwa kushirikiana na Mungu katika kazi yake ya uumbaji. Kwa hiyo, wanandoa ni wahudumu wa uhai; hilo wanalitekeleza kwa kuwapokea watoto ambao Mungu anapenda kuwajalia na kuwalea kiutu, kiimani, kimaadili na hata kitaaluma. Tukubali kwamba ndoa takatifu ni jambo zito na lenye heshima, mastahili na majukumu mazito. Licha ya kutambua hivyo, bado tunashuhudia kushamiri kwa mwelekeo wa kuchukulia ndoa kiholela na kwa wepesi mkubwa mno. Katika zama hizi, mwelekeo huo unabeba hatari kubwa kwa utakatifu, usitawi na udumifu wa ndoa. Aidha unaathiri utakatifu na uthabiti wa familia, kanisa la nyumbani. Ili kuikabili changamoto hii, ninapenda kutoa maagizo ya kichungaji kama ifuatavyo:

Katika kila parokia, iandaliwe na kuundwa timu ya kutoa mafundisho kwa ajili ya wale wanaojiandaa kwa maisha ya ndoa na hata wale ambao wameshafunga ndoa. Timu hizo ziwajumuishe wafuatao: Padre, Mganga au Nesi, Mtaalam wa Sheria, Mtaalam wa maswala ya jamii, katekista na wanandoa (mume na mke)wakomavu na  thabiti. Mafundisho yatolewe na wanajopo wote. Uwekwe muda wa kutosha kwa ajili ya mafundisho hayo. Iepukwe kabisa tabia ya kupanga mafundisho ya kurashia. Ukuu, utakatifu na umuhimu wa ndoa kama swala la maisha yote linahitaji umakini zaidi. Vijana wanaojitambua kuwa mwelekeo wao ni wa wito wa maisha ya ndoa, wajitahidi kuanza kuhudhuria mafundisho bayana mapema hata kabla hawajaanza habari za uchumba. Hilo litawasaidia kujielewa zaidi, kuyaelewa madai ya ndoa, kuelewa jinsi ya kujipanga kupata mchumba wa kufaa, kujua jinsi ya kujithibiti na kubandukana na baadhi ya mitazamo na tabia ambavyo haviakisi wito na utakatifu wa ndoa.

MIPANGO YA KICHUNGAJI & KIUCHUMI:

Mwaka huu, tulipiga hatua kubwa kijimbo kwa kukamilisha Mwongozo unaoratibu fedha na mali za kanisa. Ninaamini kwamba kila parokia ilipata nakala ya mwongozo huo. Kwa mwendo wa uwajibikaji, mpaka wakati huu, mwongozo huo unategemewa uwe umedodoswa na kuelewaka kwa wadau wengi wa kanisa. Ninafurahi kuwajulisha kwamba tayari mwongozo huo umeshatafsiriwa katika lugha ya kiswahili. Hii ni sababu tosha ya kuhimiza kwamba mapadre, watawa, kamati tendaji za maparokia, menejimenti ya asasi za kanisa, makatekisata, vyama vya kitume na vikundi vya mavuguvugu ya imani wajitume na kujitahidi kujifunza na kutekeleza mwongozo huo.

Kuanzia Januari 2016, kila mdau atapaswa kuwajibika kadiri ya mwongozo huo. Kwa kuzingatia mwongozo huo, idara za kijimbo, parokia na asasi za kanisa zijipange kuwajibika kwa njia ya ukaguzi wa vitabu vya mahesabu ya fedha (auditing). Huu ni utamaduni na uwajibikaji ambao unatupasa mbele ya wanakanisa, sheria za kanisa, sheria za nchi na mwenendo wa kujali na kuwajibika. Yawezekana baadhi wakajisikia kama vile jambo hili ni kibano kisicho na lazima wala heshima. Niseme tu kwamba hatuna budi kubadilika na kukubali kuzingatia desturi halali na bora za ulimwengu wa kitaalam (professionalism).

SALAMU ZA NOELI NA MWAKA MPYA 2016:

Wapendwa, tunahitimisha mwaka wa kanisa. Hilo litatupeleka kwenye kipindi cha Majilio ambacho kinatupatia fursa ya kujiandaa kwa Sherehe za Noeli.  Kwa moyo mkunjufu, ninapenda kumtakia kila mmoja, na wote kwa pamoja majilio mema ya wongofu na neema. Aidha ninawatakieni Heri na Baraka za Noeli. Kristu Mwokozi aliyetwaa mwili na kukaa kwetu, apate makazi mioyoni mwenu na ktika familia zenu. Awabariki, kuwafariji na kuwalinda. Mwisho, natangulia pia kuwatakia hitimisho jema la mwaka 2015, na wingi heri, baraka, neema na faraja kwa mwaka 2016. Neema na amani ya Kristo Mwokozi idumu nanyi daima.

 

Ndimi,

Wenu katika Kristo,

+ Thaddaeus Ruwa’ichi OFMCap

Askofu Mkuu wa Mwanza

Tarehe: 1 Novemba 2015

Sherehe ya Watakatifu Wote.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.