2015-12-04 15:47:00

Baraza la Kipapa la Uchumi lapongezwa na Papa Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi jioni tarehe 3 Desemba 2015 ameshikiri katika mkutano wa Baraza la Kipapa la Uchumi  na kuwaambia kwamba, anapenda kuwatia moyo wanapotekeleza dhamana na wajibu wao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa hususan katika kuangalia kwa makini miundo mbinu ya fedha na uongozi iliyoko chini ya Vatican. Baba Mtakatifu amewapongeza kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya katika kuleta mageuzi mjini Vatican ambayo yeye mwenyewe anashiriki kama nahodha wa mageuzi haya.

Kwa upande wake, Kardinali Reinhard Marx, mratibu wa Baraza la kipapa la uchumi, ameshukuru Baba Mtakatifu kwa uwepo wake katika mkutano huu pamoja na kuendelea kukazia mageuzi makubwa kuhusu masuala ya fedha, uchumi na uongozi yanayoendelea kusimamiwa na kutekelezwa na Baba Mtakatifu mwenyewe. Baraza linaendelea kuwekeza rasilimali muda na nguvu, ili kufanya tathmini na hatimaye, kuangalia sera na mikakati inayopania kukuza na kudumisha ukweli na uwazi katika masuala ya fedha na uchumi; mambo yanayogusa rasilimali ya Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.