2015-12-03 15:05:00

Tunamhitaji Papa atuimarishe katika imani, ushuhuda, malezi na uinjilishaji!


Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema hija ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika imekuwa ni kikolezo cha imani kwa watu wengi waliokuwa wamekata tamaa. Tanzania inajiandaa kuadhimisha Jubilei ya miaka 150 ya Ukristo ni kipindi ambacho kinaonesha mafanikio makubwa yaliyokwishafikiwa na Kanisa la Tanzania, lakini pia kuna shida na changamoto zake hasa kutokana na utandawazi unaowapelekea watu kuanza kusahau lile vuguvugu la Uinjilishaji lililokuwepo hapo awali. Haya yamesemwa na Askofu Ngalalekumtwa katika mahojiano maalum na Radio Vatican wakati huu Kanisa la Tanzania linapojiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya Ukristo.

Ikiwa kama Baba Mtakatifu Francisko atafanikiwa kutembelea Tanzania kunako mwaka 2018, wangependa awasaidie kukazia zaidi na zaidi dhamana na mchakato wa Uinjilishaji: utakaojikita katika katika majadiliano ya kidini na kiekumene; ushuhuda wa imani tendaji. Watanzania wasifurahie kuona Makanisa yakiwa yamefurika waamini kwani ni madogo, kumbe, bado kuna haja ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha.

Kumekuwepo na mafanikio makubwa katika uongozi wa Kanisa mahalia nchini Tanzania kwani kwa sehemu kubwa liko chini ya uongozi wa Maaskofu mahalia. Bado kuna haja ya kuhakikisha kwamba, mihimili ya Uinjilishaji inafundwa barabara, ili kweli Kanisa liweze kupata wahudumu safi na watakatifu wa Neno na Sakramenti za Kanisa; watu wenye msimamo wa maisha kadiri ya mapenzi ya Kristo Yesu. Makatekista ni wasaidizi wa karibu sana wa Mapadre, kumbe, hawa nao wanapaswa kufundwa vyema ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa kwani hii ni kazi takatifu na nyeti kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu.

Askofu Ngalalekumtwa anakaza kusema, changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, Wakleri na Watawa wanapata malezi na majiundo makini katika maisha yao ya kiroho, kiakili, kielimu na kiutu, tayari kushuhudia Kristo aliyekuwa: mtii, fukara na msafi. Wakleri na watawa wawe mfano bora wa kuigwa kwa kumwambata Bikira Maria aliyekuwa Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake. Bikira Maria ni mtawa wa kwanza aliyefungua shule ya maisha ya Yesu. Watawa wakitaka kumfahamu vyema Kristo Yesu waende kwenye shule ya Bikira Maria ili aweze kuwafunda barabara.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.