2015-12-03 10:23:00

Sikilizeni kilio cha Mama dunia!


Maadhimisho ya Kongamano la Tano la Mafundisho Jamii ya Kanisa nchini Italia yaliyokuwa yanafanyika kwenye Jimbo katoliki la Verona yamekamilika siku ya Jumapili kwa washiriki kupata ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko na Rais wa Italia Sergio Mattarella. Kwa muda wa siku tatu yaani kuanzuia tarehe 26 hadi 29 Novemba 2015 wajumbe wameangalia kwa kina na mapana kuhusu wakimbizi na historia ya kuwashirikisha katika jamii kwa kukazia umuhimu wa mafungamano ya kijamii na kifamilia.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video amewataka washiriki kusikiliza kilio cha dunia mama, ili kuweza kuheshimu viumbe hai pamoja na kumpatia sifa na heshima Mwenyezi Mungu ambaye ni Muumbaji wa vyote. Hii ndiyo changamoto kubwa anayokabiliana nayo binadamu katika ulimwengu mamboleo.

Wajumbe katika kongamano hili wamejadili pamoja na mambo mengine kuhusu: binadamu, fursa za ajira, jamii, uhuru uchumi na maendeleo. Kauli mbiu ya mwaka huu ilikuwa ni changamoto halisi za maisha mintarafu Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, Injili ya furaha “ Evangelii gaudium. Tafakari hii imeiwezesha Familia ya Mungu nchini Italia kufungua mwelekeo wa uelewa mpana zaidi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Wajumbe wanakiri kwamba, Kanisa ni mdau muhimu sana wa maendeleo nchini Italia, changamoto ni kuhakikisha kwamba, Kanisa nchini Italia linaendelea kucharukia mchakato wa maendeleo na kamwe lisikubali kubweteka, ili liendelee kuwa ni chachu ya mageuzi ya kijamii. Baba Mtakatifu anaendelea kukoleza chachu ya mabadiliko katika maisha na utume wa Kanisa kwa kujikita katika uaminifu kwa Injili ya Kristo na Kanisa lake.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.