2015-12-03 09:22:00

Jishikamanisheni na Injili ya huruma ya Mungu!


Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles linawaalika waamini kuambata Injili ya huruma ya Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Majilio, siku maalum iliyotengwa kwa ajili ya kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya waamini. Jumapili ya Biblia kwa mwaka huu ni maandalizi ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Familia ya Mungu nchini Uingereza na Walles inataka kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Biblia, maktaba maarufu kuliko zote duniani, mwaliko kwa waamini kuchota hekina na utajiri unaofumbatwa katika Maandiko Matakatifu, tayari kuumwilisha katika uhalisia maisha yao!

Maadhimisho ya Siku ya Biblia Kitaifa nchini Uingereza yanakuja siku chache tu, kabla ya Baba Mtakatifu Francisko kuzindua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu hapo tarehe 8 Desemba 2015. Maaskofu wanawataka waamini kujitosa kimasomaso ili kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu katika maisha yao, lengo ni kumkabidhi Kristo Yesu, maisha ya Kanisa na walimwengu wote, wakimwomba awamiminie neema na baraka zake kama umande wa asubuhi, ili kushiriki kikamilifu katika maboresho ya mustakabali wa taifa la Mungu.

Mwaka huu ujae huruma, ili wote waguswe na wema na upole wa Mungu, kielelezo cha uwepo endelevu wa Ufalme wa Mungu kati ya watu wake! Baada ya kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao; wajitahidi kuwa ni vyombo na watangazaji wa Neno la Mungu kwa kuwa na ari na mwamko wa kimissionari, tayari kuwashirikisha hata wasio amini Habari Njema ya wokovu, chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani. Waamini katika ngazi mbali mbali wanahamasishwa kutafakari jinsi ambavyo kweli wanaweza kuwa ni zawadi ya Neno la Mungu kwa jirani na ndugu zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.