2015-12-03 12:03:00

Funguka! Chukua hatua mlinde mtoto apate elimu!


Ifuatayo ni hotuba iliyotolewa hivi karibuni na Chiku Galawa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Tanzania katika maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na watoto mkoa wa Dodoma, tarehe 25 Novemba 2015 na kilele cha maadhimisho haya ni hapo tarehe 10 Desemba 2015. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Funguka! Chukua hatua mlinde mtoto apate elimu”. Awali ya yote napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa kunialika na kunipa heshima ya kuwa mgeni Rasmi katika hafla hii ya ufunguzi wa Siku 16 za Maadhimisho ya kupinga Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia na watoto katika Mkoa wetu wa Dodoma.  Pili natoa shukurani za dhati kwa Washiriki wote na Kamati ya maandalizi kwa kazi nzuri mliyoifanya pamoja na wadau wote mlioacha shughuli zenu kuungana na dunia nzima kupaza sauti zenu na kutoa ujumbe wenu kwa watu wote Kupinga aina zote za Ukatili na Unyanyasaji wa kijinsia na watoto.

Ndugu wananchi;

Sisi wana Dodoma pamoja na Taifa letu tunaungana na dunia nzima kufanya maadhimisho ya siku 16 ya kupinga Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia ambayo huadhimishwa kila mwaka kwa siku 16 kuanzia tarehe 25 Novemba hadi tarehe 10 Desemba. Kauli mbiu yetu ya mwaka huu ni “FUNGUKA! CHUKUA HATUA MLINDE MTOTO APATE ELIMU”. Kauli mbiu hii inatujengea uwezo na ufahamu wa kina ya kwamba msingi wa mabadiliko kitabia, makuzi bora ya watoto, ndoto njema, dira njema inaanza katika familia. Mtoto akipata malezi bora na Elimu bora inamjengea uwezo wa kujitambua na kuwa shujaa na kuwa na mwanzo ulio bora wa kukabiliana na changamoto za maisha.

Ndugu wananchi; Maadhimisho haya yanatoa fursa kwa jamii kujifunza, kuelewa na kuchukua hatua dhidi ya vitendo viovu vya Ukatili na Unyanyasaji wa kijinsia na watoto. Tunapofanya maadhimisho haya kwa vitendo ni kupaza sauti zetu tunaojitambua kuwafichua wahalifu wote na kuhakikisha kwamba familia zetu ni salama na zenye ustawi bora. Wana Dodoma tutumie siku hizi 16 za kupinga Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia na watoto kuleta mabadiliko ya kweli, kutambua aina zote za ukatili katika familia zetu na kuchukua hatua kuzitokomeza.

Ndugu wananchi; Tatizo la Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia lipo na linaendelea kuathiri watu wengi hasa wale walio katika makundi maalum yanayoonewa kama Wanawake, Watoto, Walemavu na Wazee. Vitendo vya ukatili wa kijinsia vina athari nyingi kwa jamii zikiwemo athari za Kiafya, Kijamii, Kiuchumi, Kisaikolojia na hata Kisiasa. Kupitia maadhimisho haya naamini wananchi tutapata ufahamu wa kutosha kupitia midahalo, elimu kupitia redio mbalimbali za hapa Dodoma, kuwatembelea watoto waishio kwenye mazingira magumu, kukutana na watu wenye ulemavu na kutambua aina mbalimbali za Ukatili na Unyanyasaji na kuchukua hatua zinazostahili pale yanapojitokeza.

Ndugu wananchi; Watu waliofanyiwa Ukatili wa aina yoyote huendelea kuwa wanyonge maisha yao yote na athari hizo huwatesa maisha yao yote vizazi hadi vizazi. Mfano mzuri ni ongezeko la watoto wanaoishi mitaani na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi, watoto hawa maisha yao hayawezi kuwa na furaha kwani hawatapati fursa za Elimu, matibabu, malezi bora na mwisho wa maisha yao ni mateso. Wengine huzama katika maisha hatarishi ya ukahaba, utumiaji madawa ya kulevya na ujambazi hata vizazi vyao vinaendelea kurithi mateso hayo.

Ndugu wananchi; Niwajibu wa kila mmoja kulaani na kupinga vikali ukatili wa kijinsia, toa taarifa kwa vyombo husika na Jeshi la Polisi ili hatua ziweze kuchukuliwa haraka. Ifahamike kuwa jukumu la kupambana na makosa ya ukatili wa kijinsia si la mtu mmoja, Asasi au Taasisi fulani bali ni jukumu la Jamii nzima. Kila mtu aguswe katika nafsi yake kutokomeza ukatili. Vitendo vya Ukatili wa kijinsia vinafanyika Majumbani mwetu ndani ya familia, mitaani na mahali popote pale vyaweza kutokea. Vyanzo vya ukatili majumbani vinasababishwa na matumizi ya pombe kupindukia, madawa ya kulevya, mila potofu na umasikini uliokithiri. Moja ya watekelezaji wa ukatili huo yaweza kuwa mzazi mmoja au wazazi wote, wanafamilia, majirani, makundi ya watu na waajiri wa wafanyakazi majumbani.

Ndugu wananchi; Natambua kuwa kwa nafasi na nyakati tofauti; Taasisi mbalimbali za Umma, Vyombo vya dola, Mashirika yasiyo ya kiserikali, Taasisi za Dini na Afya wamekuwa wakifanya jitihada nyingi katika kuhakikisha Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia unapungua ili kuwa na jamii inayostawi vizuri. Juhudi hizi yafaa kuungwa mkono na watu wote kwani jamii inapoharibika watu wote tusitegemee kuwa salama. Pia Serikali inatambua na kuthamini michango ya wadau binafsi na tasisi zote zinavyoshiriki kwa vitendo kupinga Ukatili na Unyanyasi wa Kijinsia na Watoto kama tunavyoona mlivyoshirika hapa leo; tuendelee kuisaidia jamii kwa pamoja kutokomeza unyanyasaji na Ukatili wa Kijinsia.

Ndugu wananchi;

Nimatarajio yangu kwamba tunapofanya maadhimisho haya ya siku 16 tunataarajia kwamba jamii itajitokeza bila woga kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali za mitaa, ustawi wa jamii na Polisi ili kufichua makosa ya Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia na Watoto. Aidha ni nipo taayari kupokea taarifa za siri dhidi ya matukio haya,iwapo mtoa taarifa huyo ataona ana wasiwasi au bado haamini mabadiliko makubwa ya kiutendaji ndani ya ngazi nilizozitaja na Jeshi la Polisi. Naagiza watendaji waliyo chini yangu kufanya hivyo pale mtoa taarifa za siri anapoomba msaada huo. Ukatili na unyanyasaji wa Kijinsia ni Uhalifu ambao kamwe haukubaliki. Matarajio yangu kuona kwamba ushughulikiaji wa makosa haya unafanyika kwa Haki na hatua zinachukuliwa haraka kwa mujibu wa sheria za nchi. Matokeo mazuri ya ushughulikiaji makosa ya aina hii yatakuza uelewa kwa jamii kufichua uhalifu huo na hatimaye uhalifu wa aina hiyo kumalizika na kuwa na Jamii bora isiyo na ukatili na unyanyasaji .

Ndugu wananchi; Natoa wito pia kwa Wanahabari kutumia kalamu zenu na kamera zenu kufichua popote walipo wahalifu wa makosa haya. Wanaharakati wa Haki za Binadamu popote mlipo mpaze sauti kupinga na kufichua matendo yote ya manyanyaso na ukatili wa Kijinsia na Watoto. Natambua na nathamini mchango wa viongozi wetu wa dini, wahanga ni waamiini wenu na hata wahalifu nao ni waumini wenu pia. Mkitukanya wote mtakuwa mmetusadia kujenga Jamii Bora isiyokuwa na wanyanyasaji. Aidha Serikali za Mitaa nazo zishiriki kikamilifu kwani ndiyo wapo karibu zaidi na wananchi.

Mwisho: Kwa hotuba hii fupi natamka kuwa NIMEFUNGUA RASMI maadhimisho ya siku 16 za kupinga Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia na watoto mkoani Dodoma. “FUNGUKA! CHUKUA HATUA MLINDE MTOTO APATE ELIMU”.








All the contents on this site are copyrighted ©.