2015-12-02 10:31:00

Kutana na vigogo wa dunia, lakini itifaki imezingatiwa!


Katika mkutano rasmi kuna utaratibu wa kutambulishana kwa kuzingatia protokali. Katika utambulisho hutolewa pia wasifu wa mgeni mwalikwa. Hatimaye hutolewa mada ya mkutano. Injili ya leo inamtambulisha mtambulishaji. Mwinjili anamtambulisha Yohane Mbatizaji ambaye ni mtambulishaji wa  mgeni tunayemsubiri yaani Yesu Kristo. Yohane anatambulishwa kwa mbwembwe wakitajwa vigogo saba wa serikali na dini walioishi wakati wake. Kigogo wa kwanza ni Kaisari Tiberio: “Mwaka wa kumi na tano wa kutawala kwake Kaisari Tiberio,” (Lk. 3:1). Mama ya Tiberio alikuwa Livia.

Mwaka wa kumi na nne baada ya Kristu Kaisari Augusto alimchukua Livia kuwa mke wake wa tatu na akamrithi Tiberio kama mtoto wa kambo. Augusto alipokufa Tiberio akarithi kiti cha kifalme. Kwa hiyo ukijumlisha “Mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio”  uliosemwa, na ile miaka kumi na nne aliporithiwa Tiberio unapata jumla ya miaka ishirini na tisa baada ya Kristu. Lakini kwa Waasiria walihesabu miaka tofauti, yawezekana bado tuko miaka ya ishirini na saba baada ya Kristo. Kwa hiyo miaka hii inaweza kutusaidia kukadiria kipindi cha maisha ya Yesu hadharani, na kwamba aliishi hadi mwaka wa thelathini baada ya Kristo.

Kigogo wa pili ni “Pontio Pilato.” Huyu alikuwa liwali wa sita wa Uyahudi kuanzia mwaka wa ishirini na sita hadi thelathini na saba. Hivi alitawala karibu kipindi chote cha maisha ya hadharani ya Yesu. Kadiri ya utafiti wa Filone, yasemwa kwamba Pilato alikuwa na msimamo migumu, mwenye kiburi, mkali, mwenye majivuno, msharati mkubwa, mwonevu, anatoa hukumu bila kuhoji watuhumiwa. Alikuwa anakaa Kaisaria lakini nafasi hii alipokuwa Yerusalemu kwa Sikukuu ya Pasaka ndipo alipoletewa kesi ya Yesu ya kumhukumu kufa.

Kigogo wa tatu ni “Herode Mfalme wa Galilaya” yaani Herode Tetraka, lakini jina lake halisi ni Antipa. Mji wake mkuu ulikuwa karibu na Nazareti alipoanzia utawala. Mwaka wa ishirini na sita akahamishia makao yake kando ya ziwa Tiberio. Huyu Antipa ndiye aliyelipa ziwa hilo jina la Tiberio. Kipindi cha utawala wa Herode Antipa Yesu alikuwa amejizamisha kabisa katika kazi. Kigogo wa nne ni “Filipo, ndugu yake mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti.” Huyu Filipo alikuwa kaka ya Herode Antipa mtoto wa Herode Mkuu, aliyekuwa anatawala Kaisaria Filipo unapoanza mto Yordani. Huko aliishi na mke wake Salome yule maarufu wa kucheza mauno hata akasababisha mfalme apoteze kichwa, na kupelekea kupoteza kichwa cha Yohane.

Kigogo wa tano anayetajwa hapa ni Lisania mfalme wa Abilene. Kigogo huyu hajulikani sawasawa habari zake.  Baada ya kuwaorodhesha vigogo hawa watano, kwa kuzingatia itifaki, Mwinjili anaongeza tena vigogo wawili wote wakiwa ni Makuhani. Ingawa ingetosha kumtaja kuhani mmoja tu yaani Kaifa aliyekuwa kuhani mkuu wakati ule, lakini anamtaja pia Anas aliyekuwa mkwe wa Kaifa.  Orodha ya vigogo hawa saba siyo ya bure, wala haba kama kiatu cha raba! Bali ni kama kigezo na hoja ya umuhimu wa ujumbe tutakaoletewa. Mosi Mwinjili anatuonesha ukuu wa Yohane Mbatizaji, akithibitisha kuwa ujumbe na utambulisho atakaotoa siyo hadithi za pwagu na pwaguzi bali ni ujumbe wa kihistoria na yeye ndiye mtambulishaji rasmi wa Mkombozi ajaye. Kwa hiyo, Yohane mbatizaji ni mtu wa historia aliyeishi kweli wakati huu ambapo vigogo hawa walikuwa wanaishi.

Pili, namba hii inaonesha kuwa historia inahusisha watawala wa serikali na siasa yaani Tiberius, Pilato, Herode, Filipo, Lisinia na inahusisha pia historia nzima ya utawala wa kidini inayowakilishwa na makuhani wakuu Anas na Kayafa. Kwa hiyo ujio wa Mungu katika ulimwengu huu unawahusu binadamu wote na utawaathiri watawala wote. Tatu, yataka kuonesha kwamba ufalme utakaozinduliwa na Yesu kwa maisha yake siyo kitu kigeni bali ni ufalme wa ulimwengu huu, lakini sasa hautaongozwa tena kwa vionjo na upumbavu wa kibinadamu bali utaongozwa na sheria ya haki na upendo wa Kimungu unaogusa maisha ya kawaida ya kila siku ya binadamu.

Baada ya kuona historia hiyo ya mambo ya binadamu yalivyokuwa hapa duniani, sasa linashuka Neno la Mungu litakalobadilisha historia ya ulimwengu kama ilivyoandikwa: “Neno la Mungu lilimfikia Yohane, mwana wa Zakaria, jangwani.” Ujumbe au Neno hilo haliwafikii watawala wakaao Ikulu na wenye vyombo vya dola kwa mawasiliano wanaokula “Bata kwa mrija” bali Neno linamwendea Yohane mwana wa Zakaria aliyekuwa jangwani, kwenye upweke na mapambano makali ya kiroho na kimwili. Hapa linatajwa jangwa kwa sababu Yohane alikuwa mtoto wa kuhani Zakaria. Kwa kawaida kadiri ya mapokeo mtoto wa kuhani alitakiwa kurithi mikoba ya baba yake na kuwa kuhani ili kuadhimisha Ibada na Liturujia.

Lakini, kutokana na lugha yake, yaonekana Yohane alikuwa anakaa jangwani (upwekeni) katika monasteri ya watawa wa Kumrani. Watawa hao waliutoroka mji wa Yerusalemu kwa sababu waliona makuhani wake walikuwa mafisadi na wala rushwa, watu waliokuwa wanachakachua sadaka za wanyonge, na kufanya ibada za kinafiki Hekaluni. Wakaona afadhali kujitenga pembeni na kujiandaa kwa ujio wa Bwana. Kadhalika maisha ya jangwani ni ya kawaida na ya mambo machache. Jangwa linatualika kuishi maisha ya kawaida kwa sababu ulimwengu umesheheni mambo yanayozuia tusione mambo muhimu.

Ulimwengu umejaa: dhukuma, nyanyaso, vita, uonevu, ubabe, mauaji na mambo mengi yasiyovumilika. Kwa hiyo, tunaletewa Yohane Mbatizaji ili kutuandaa kuukaribisha ulimwengu mpya unaoletwa na Yesu, kwa maisha na maneno yake anatuambia jinsi ya kumruhusu Bwana kuingia katika ulimwenguni huu. Aidha, jangwani kuna unyamavu mkuu kwani mazingira yake ni tofauti na yale ya wanaopiga makelele na kugomba, kuamrisha wengine na kuonesha ubabe na utawala kwa kupandishana sauti. Yesu anapenda kukaa mahali penye unyamavu, maelewano na amani.  Baada ya kumwona mtu aliyepokea Neno na mahali alipokaa sasa tunaambiwa kazi yake. Yohane “Akafika nchi yote iliyo karibu na Yordani, akihubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi.” (Lk 3:3). Kumbe, kazi ya Yohane siyo kubatiza, bali kuhubiri. Yohane alihubiri Ubatizo wa ondoleo la dhambi, yaani kugeuka, kuongoka na kubadili fikra. Kuingia majini kulikofanyika baadaye kulikuwa ni alama ya nje ya kujisafisha dhambi. Kwa hiyo Yohane ni mwandalizi wa mazingira kabla ya ujio wa mgeni rasmi atakayebadili historia.

Sasa angalia kwa makini sana. Luka anahitimisha fasuli yake kwa nukuu toka Nabii Isaya wa pili wanayofanya Wainjili wote wanne: “Kila bonde litajazwa, na kila mlima na kilima kitashushwa; palipopotoka patakuwa pamenyoka, na palipoparuza patalainishwa” (Isaya 40:3-4). Maana yake, huu ni mwisho wa historia ya kale, kwani sasa Mungu mwenyewe atakuja na kufuta kila kitu kinachozuia binadamu kutoonana na Mungu. Ataondoa vikwazo vyote vilivyokuwa vinaletwa na wale vigogo saba. Lakini Luka anaendelea kunukuu aya ya tano ya Isaya ambayo wainjili wengine wameacha kuinukuu. Aya hiyo ndiyo iliyojaa uhondo ambao ni kiini cha wazo kuu la Injili ya leo. Tangazo hilo linaloleta furaha kuu ni: “na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu.” (Lk. 3:6). Yaani wokovu wa kila mtu umeanza kwa utambulisho wa Yohane mbatizaji, halafu unahitiishwa na mgeni rasmi ajaye yaani Yesu Kristo.

Ndugu zangu, leo tumetambulishwa rasmi ujio wa Habari njema ya upendo wa Mungu katika historia ya ulimwengu huu. Habari hiyo inawaji wote wenye mwili. Tujiandae kuupokea kwa furaha na kutengeneza mazingira safi katika sakafu ya mioyo yetu! Mgeni anayekuja ni Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai, anataka kufanya makazi katika maisha yako! Jaribu kumpatia nafasi!

Na Padre Alcuin Nyirenda!








All the contents on this site are copyrighted ©.