2015-12-01 12:07:00

Siku ya Ukimwi Duniani kwa Mwaka 2015


Wito unatolewa kwa wananchi kote nchini Tanzania kuyatumia maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Desemba 1 ya kila mwaka kupima afya zao ili kudhibiti maambukizi mapya ya VVU. Akizungumza na waandishi wa Habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI nchini Tanzania Dkt. Fatma Mrisho amesema Siku ya Ukimwi Duniani nchini inaadhimishwa kwa kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao na kupata elimu ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

Ameeleza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanaambatana na shughuli mbalimbali zikiwemo za Utoaji wa Elimu ya Afya na Upimaji wa hiari wa VVU katika maeneo mbalimbali kote nchini kupitia vituo vilivyowekwa, Kufungua kituo cha maarifa cha udhibiti UKIMWI eneo la Manyoni mkoani Singida ambayo ni njia kuu kuelekea mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi za Jirani za Burundi na Rwanda.

Ameongeza kuwa Tume kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendesha mikutano ya kitaalam kuhusu UKIMWI, Zoezi la upimaji wa hiari wa VVU kwa wananchi, Kupokea tamko litakalotolewa na Baraza la Watu wanaoishi na VVU pamoja na Uzinduzi wa taarifa ya tathmini ya Sheria zinazotumika zinazohitaji kurekebishwa zinazozuia malengo ya sifuri 3. Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi iwe ni chachu ya kupunguza maambukizi mapya ya UKimwi nchini Tanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa ufuatiliaji na tathmini kuhusu UKIMWI wa TACAIDS Dkt.Jerome Kamwela amesema kuwa kiwango cha maambukizi ya UKIMWI kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2011/2012 kimepungua na kufikia asilimia 5.3 huku mikoa ya nyanda za juu kusini ya Njombe, Iringa na Mbeya ikiongoza kwa kuwa na maambukizi zaidi na mikoa ya Manyara, Tanga na Lindi ikiwa na maambukizi ya chini ya asilimia mbili. Dkt. Kamwela amesema kuwa maambukizi ya VVU ni mengi hasa kwa kundi la watu wenye umri wa miaka 19-24 huku makundi ya wanaojidunga, wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja, wanawake wanaofanya biashara ya ngono yakiendelea kuwa katika hatari ya kuathiriwa zaidi na maambukizi ya VVU.

Na Mwandishi maalum.








All the contents on this site are copyrighted ©.