2015-12-01 08:59:00

Papa: Hata katika umaskini wao, Waafrika daima ni watu wa furaha! Wamenikuna!


Baba Mtakatifu Francisko amerejea mjini Vatican baada ya kuhitimisha hija yake ya kitume Barani Afrika alikotembelea Kenya, Uganda na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kuanzia tarehe 25 hadi 30 Novemba 2015. Huko amepata nafasi ya kujionea na kusikiliza kilio cha Familia ya Mungu kuhusiana na umaskini, ukosefu wa haki msingi na mahitaji muhimu ya binadamu. Ameguswa na kilio cha vijana wanaotaka saratani ya rushwa na vitendo vya kigaidi, uharibifu wa mazingira ipewe tiba muafaka; mambo yote haya yanahatarisha utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu akiwa njiani amepata fursa ya kujibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake. Anasema, pale ambapo sera za uchumi na maendeleo zinajikita katika ubinafsi, utajiri na mali, hapo utu na heshima ya binadamu viko rehani. Inasikitisha kuona kwamba, kuna watu wachache sana wanaomiliki utajiri wa dunia wakati ambapo kuna kundi kubwa la watu bado linaendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini na magonjwa.

Baba Mtakatifu anasema, amesikitishwa sana na mahangaiko ya wananchi  wa kitongoji cha Kangemi, Kenya; ameguswa na mateso ya watoto waliolazwa kwenye Hospitali ya Watoto Bangui. Amejionea jinsi watoto wanavyoteseka kutokana na utapiamlo mkubwa, kwa kukosa dawa na vifaa tiba. Yote haya ni kwa sababu watu wanapenda kuabudu fedha na mali kuliko utu na heshima ya binadamu. Magonjwa, umaskini na maafa yataendelea kuwaandama wanadamu ikiwa kama binadamu mwenyewe hataweza kufanya toba na kumwongokea Mungu. Matajiri wawe na ujasiri wa kugawana rasilimali ya dunia na maskini, ili waweze wao pia kufurahia Injili ya maisha!

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, ameguswa kwa namna ya pekee na ukarimu, furaha na maisha ya Familia ya Mungu Barani Afrika hata katika umaskini wao, bado wanaweza kufurahia maisha. Wameonesha ukarimu wa ajabu kwa kujitokeza kwa wingi kumpokea na kumsikiliza. Kenya inaonekana kuwa na maendeleo; Uganda bado inajikita katika mashuhuda wa imani; huu ndio utambulisho wao unaowapatia ujasiri wa kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo! Katika Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Baba Mtakatifu anakaza kusema, wao wana kiu ya amani, upatanisho na msamaha wa kweli; udugu, umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kutambua kwamba wao ni ndugu wamoja! Waamini wanapaswa kuwa wajenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu na wala si wachochezi wa kinzani na misigano mambo ambayo yanasigana na imani wanayoiungama. Serikali ya mpito Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati isaidie kuwapatia wananchi: haki, amani, msamaha na upatanisho wa kitaifa.

Bara la Afrika lina utajiri na raslimali nyingi; lina tunu na tamaduni zinazopaswa kuendelezwa. Kwa bahati mbaya Bara la Afrika linaonekana na wengi kuwa ni uwanja wa fujo pasi na usalama. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Bara la Afrika limekuwa kama kichwa cha mwendawazimu, watu wengi wanalinyonya kiasi kwamba limekuwa ni shahidi wa unyonyaji pasi na huruma. Anasema analipenda Bara la Afrika na kwamba, kuna haja ya kushikamana ili kuliendeleza Bara la Afrika badala ya kuendelea kunyanyaswa na wenye nguvu wachache duniani!

Baba Mtakatifu anawataka waandishi wa habari kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kuzingatia kanuni, maadili na sheria kwani hakuna uhuru pasi na mipaka hata katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ambao umeenea sehemu mbali mbali  za dunia hata mjini Vatican. Vyombo vya habari viwe na ujasiri wa kufunua maovu na vyombo vya sheria vitekeleze wajibu wake barabara.Waandishi wa habari waseme ukweli pasi na kuuvuruga kwa ajili ya mafao yao binafsi; waoneshe weledi katika kazi zao kwa kujikita katika ukweli pamoja na kuheshimu sifa ya mtu! Waandishi wa habari wawe na ujasiri wa kuomba msamaha pale wanapokosea na kukiuka kanuni maadili za kazi. 

Katika mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi na misimamo mikali ya kidini, viongozi wa kidini wanapaswa kutekeleza dhamana na wito wao kwa kutambua kwamba, wao ni vyombo na wajenzi wa: umoja, haki, amani,upatanisho na maridhiano. Misimamo mikali ya kidini ni saratani ambayo iko katika dini zote na inakwenda kinyume kabisa cha mafundisho msingi ya kidini. Hapa kuna watu wanatumia misimamo mikali ya kidini kwa ajili ya mafao ya binafsi, ili kujipatia fedha na utajiri wa haraka haraka.

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, kumekuwepo na tatizo la kumshirikisha Monsinyo Vallejo Balda pamoja na Francesca Immaculata Chaouqui katika Tume ya Marekebisho ya masuala ya uchumi na fedha Vatican, ingawa baada ya kumaliza kazi zao waliondoka na kwamba, watuhumiwa hawa hawakumnyima usingizi hata kidogo kwani kile kilichochapishwa kwenye vitabu kinaonesha kazi ya mageuzi iliyofanywa. Rushwa anakaza kusema Baba Mtakatifu ni adui wa haki. Mapambano dhidi ya rushwa mjini Vatican ni mchakato ulioanzishwa na Kardinali Joseph Ratzinger wakati alipotoa tafakari ya Njia ya Msalaba, siku chache kabla ya kifo cha Papa Yohane Paulo II, akachaguliwa na Makardinali kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kuendeleza mchakato wa mageuzi.

Kumbe, wizi wa nyaraka za siri kutoka Vatican ni tendo la jinai na kwamba, Baba Mtakatifu angependa kesi hii iwe imekamilika na kutolewa hukumu kabla ya kuanza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, hapo tarehe 8 Desemba 2015, pengine jambo hili halitawezekana anasikitika kusema Baba Mtakatifu Francisko na kwamba kwa kushirikiana na Makardinali wataendelea kufanya mageuzi kadiri ya maelekezo yaliyotolewa na Makardinali katika mikutano yao kabla ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kunako mwaka 2013.

Kuhusu Ugonjwa wa Ukimwi ambao bado unaendelea kusababisha vifo vingi miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa litaendelea kuhimiza kanuni maadili na utu wema; kwa kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Matumizi ya kondomu si dawa ya kuzuia matatizo na majanga yanayoliandama Bara la Afrika. Kuna ukosefu wa haki msingi za binadamu; uharibifu mkubwa wa mazingira; baa la njaa na utapiamlo; ukosefu wa maji safi na salama; bado kuna biashara kubwa ya silaha, unyonyaji na udhalilishaji wa binadamu; watu hawana makazi bora na salama. Matatizo na changamoto hizi zikipewa ufumbuzi muafaka hata Ukimwi utatoweka.

Baba Mtakatifu anasema aliwaahidia Mapatriaki wa Armenia kushiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 101 ya mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Armenia. Lakini ikumbukwe kwamba, vita ni kiwanda kinachozalisha silaha na utajiri kwa watu wachache, hata katika nchi zile ambazo uchumi wake unachechemea, bado utakuta wananunua silaha za mapambano! Vita ni dhambi dhidi ya ubinadamu na madhara yake ni makubwa licha ya vifo na maafa; vita inasababisha pia biashara haramu ya binadamu, udhalilishaji wa utu na heshima ya binadamu bila kusahau unyonyaji. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, vita inasitishwa ili amani iweze kutawala katika akili na mioyo ya watu. Mwenyezi Mungu ndiye asili ya amani changamoto kwa watu wote kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumzia kuhusu mazingira anakaza kusema, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanaoshiriki katiki katika mkutano wa athari za mabadiliko ya tabianchi, Cop21 huko Paris, Ufaransa wanao wajibu mkubwa kuhakikisha kwamba kunakuwepo na udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi vinginevyo, dunia itaendelea kushuhudia maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu anasema, ana imani na matumaini kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kwamba, wataweza kutoa majibu muafaka kuhusiana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Dini ya Kiislam ina tunu msingi za maisha ya kiroho zinazoweza kutumika katika mchakato wa majadiliano ya kidini katika ujenzi wa udugu na urafiki; maisha ya kiroho yanayojika katika mambo msingi badala ya kushabikia misimamo mikali ya kidini ambayo inapatikana katika dini zote. Hii ni changamoto kwa waamini kutubu, kuongoka na kuomba msamaha, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Baba Mtakatifu anasema katika umri wake, safari ndefu ni taabu na shida anatarajia kwenda nchini Mexico ili kutoa heshima yake kwa Bikira Maria pamoja na kutembelea baadhi ya maeneo ambayo hayajawahi kutembelewa na Mapapa. Kunako mwaka 2017 tayari amekwisha kupata mwaliko wa kutembelea baadhi ya nchi za Amerika ya Kusini. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru waandishi wa habari wote waliokuwa kwenye msafara wake Barani Afrika kwa kazi kubwa waliyoifanya ili kuwahabarisha watu. Amewashukuru kwa maswali yao na kwamba, ameyajibu kadiri anavyofahamu pale ambapo haja jibu amewaambia wazi wazi na wala si sehemu ya utamaduni wake kuficha mambo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.