2015-12-01 10:57:00

Falsafa ya kushukuru ni kuomba tena!


Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada ya kuwasili mjini Roma na kutua kwenye Uwanja wa ndege wa Ciampino majira ya saa 12:30 za jioni alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma ili kumshukuru Bikira Maria kwa ulinzi na tunza yake ya kimama. Itakumbukwa kwamba, hata kabla ya kuondoka, siku iliyotangulia alikwenda kusali na kujikabidhi nchini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Baba Mtakatifu alionekana kuchoka lakini akiwa amejaa furaha kubwa moyoni mwake kwa kukutana na kuonja ukarimu wa Familia ya Mungu Barani Afrika.

Wachunguzi wa mambo wanasema, Kanisa la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma, tangu Baba Mtakatifu Francisko achaguliwe ametembelea Kanisa hili mara 28 kwa nyakati tofauti lakini hasa zaidi kabla ya kuondoka na anapohitimisha hija zake za kitume sehemu mbali mbali za dunia. Utamaduni wa kushukuru umejikita katika maisha na moyo wa Baba Mtakatifu Francisko tangu asubuhi ya tarehe 14 Machi 2013 siku moja tu baada ya kuchaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Jamani, falsafa ya kushukuru ni kuomba tena!

Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.