2015-11-30 09:50:00

Vijana msikimbie magumu na changamoto za maisha! Simameni imara!


Baba Mtakatifu Jumapili jioni tarehe 29 Novemba 2015, ametoa Sakramenti ya Upatanisho, kwa mwaliko kwa waamini kutubu na kumwongokea Mungu, ili waweze kujipatanisha na jirani zao; tayari kuambata amani na huruma ya Mungu katika maisha yao, tayari kushuhudia utakatifu wa maisha. Hii ni safari ya mabadiliko ya kiroho na kimwili. Kwa wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati mgomba ni alama ya nguvu na lishe bora.Baba Mtakatifu kabla ya kuanza mkesha wa sala amewakumbusha kwamba, mgomba nchini mwao ni alama ya matumaini na nguvu, kwani mgomba unawawezesha kupata ndizi, chakula muhimu kwa maisha yao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, vijana katika kipindi hiki wanakabiliwa na changamoto ya vita, chuki, mipasuko ya kisiasa, kijamii na kidini; changamoto ni kusimama kidete kuondokana na kishawishi cha kutaka kukimbia matatizo, bali kusimama kidete kutetea mafao ya wengi. Vijana waoneshe ujasiri wa kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto mbali mbali za maisha. Silaha yao ya kwanza iwe ni sala kwani ina nguvu ya kushinda ubaya na hivyo kuwawezesha kumkaribia Mwenyezi Mungu. Vijana wajenge na kuimarisha moyo wa sala!

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, jambo la pili ni kuwa wajenzi na mashuhuda wa amani inayopaswa kufanyiwa kazi kila siku ya maisha. Amani haiwezi kujengwa kwa mtutu wa bunduki! Ili kujenga amani ya kweli, vijana wanapaswa kuondokana na chuki pamoja na uhasama, tayari kusamehe na kusahau. Kwa njia hii vijana wanaweza kuwa washindi wa mapendo katika vita ngumu ya maisha! Inawezekana kabisa kumsamehe na kumpenda adui na kwa njia hii wanakuwa kweli mashuhuda wa amani inayomwilishwa katika upendo, msamaha na upatanisho.

Baba Mtakatifu amekamilisha Katekesi yake kwa kuwataka vijana kuwa na ujasiri wa kushinda kishawishi cha kutaka kukimbia matatizo, wawe na ujasiri wa kusamehe na kuwa ni wajenzi wa upendo na amani. Lango la Jubilei ya huruma ya Mungu limefunguliwa, mwaliko kwa waamini kujiaminisha kwa huruma ya Mungu, kwani Mungu ni upendo na chemchemi ya amani ya kweli. Vijana waendelee kusali ili waweze kusamehe, kupenda na hatimaye, kuwa kweli ni wajenzi wa amani.

Baba Mtakatifu katika mahubiri aliyokua ameandaa na baadaye kumpatia Askofu mkuu Dieudonnè Nzapalainga, Baba Mtakatifu amekazia mambo makuu matatu: ujasiri wa kuvuka mambo ya zamani; toba na msamaha pamoja na kuanza njia mpya ya maisha. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuuvua utu wa kale na kuanza kutembea katika njia mpya ya maisha kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.Huruma na msamaha wa Mungu unawawezesha waamini kuwa na moyo wa amani unaothubutu kusamahe wale wanaowakosea.

Baba Mtakatifu ameonesha moyo wa upendo na mshikamano kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na: vita, machafuko ya kidini, kisiasa na kijamii nchini humo. Mwenyezi Mungu anawajalia daima nguvu ya kuwa ni vyombo na wajenzi wa haki, amani na upatanisho nchini mwao.  Vijana wanaendelea kuhamasishwa kujenga mahusiano mema na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala na Tafakari ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa, ili Yesu aweze kuwaangazia katika mapito ya maisha yao na kupendana kama ndugu na kwamba, tofauti zao ni utajiri mkubwa. Vijana wanakumbushwa kwamba, amani ni mchakato endelevu unaofanyiwa kazi kila kukicha na hapa hakuna kulala hadi kieleweke!

Baba Mtakatifu anasema amani inajikita katika njia ya huduma, unyenyekevu pamoja na kuguswa na mahitaji ya jirani ndani ya jamii. Hizi ni tunu msingi na chemchemi ya matumaini ya Kikristo wanapojiandaa kuvuka kwenda upande wa pili wa mto! Kauli mbiu inayoongoza hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Vijana waendelee kushikamana na Yesu katika maisha ya familia na nchi yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.