2015-11-30 09:25:00

Papa Francisko ameonesha ujasiri wa imani dhidi ya woga usiokuwa na mashiko!


Hija ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati ni kielelezo cha ushindi wa imani dhidi ya woga na wasi wasi usiokuwa na tija wala mashiko. Ni ushindi unaofumbata huruma na mshikamano wa Kanisa la Kiulimwengu. Vita, machafuko ya kisiasa na kidini, wasi wasi na vurugu ni mambo ambayo hayakumkatisha tamaa Baba Mtakatifu Francisko kutembelea Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Ameonesha ujasiri na dhamiri nyofu, fundisho makini kwa watu wote.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Mama Catherine Samba-Panza Rais wa serikali ya mpito jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, wakati wa hotuba ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini mwake. Rais ameomba msamaha kwa niaba ya Serikali, wanasiasa na watu wote waliochechea machafuko ya kisiasa na kidini na hivyo kupelekea mauaji ya watu wasiokuwa na hatia sanjari na uharibifu mkubwa wa nyumba za ibada na makazi ya watu! Umefika wakati wa kuomba na kutoa msamaha ili Afrika ya Kati iweze kuanza tena safari ya maisha mapya ya kiroho yanayofumbata upendo.

Rais Samba-Panza anakaza kusema, zawadi kubwa ambayo Baba Mtakatifu Francisko amewapelekea nchini mwao ni sala na maombi ili Shetani ambaye ni chanzo cha kinzani na migawanyiko kati ya watu aweze kushindwa na kutoweka nchini humo, ili watu waweze kupendana, kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu. Ni matumaini ya wananchi wa Afrika ya Kati kwamba, amani, utulivu na usalama vitaweza kurejea tena, ili mchakato wa demokrasia uweze kusonga mbele. Ili kufanikisha yote haya kuna haja ya kuondokana na chuki, uhasama, migawanyiko, ubaguzi wa kidini na kikabila. Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati wanapaswa kuondokana na matumizi ya silaha na nguvu, ili wananchi waweze kushirikiana katika ujenzi wa nchi yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.