2015-11-30 09:37:00

Papa Francisko afungua lango la Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, Bangui


Katika maadhimisho ya Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio Mwaka C wa Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko akiwa kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ili kuzindua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu kabla ya kufungua lango kuu la Jubilei amewaambia waamini waliokuwa wamekusanyika kwa wingi Kanisani hapo kwamba, Bangui umekuwa ni mji mkuu wa maisha ya kiroho duniani, kwani uzinduzi wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu unafanyika mjini hapo kama sehemu ya utangulizi wa tukio hili kubwa la kiimani.

Hii ni nchi ambayo inateseka kwa miaka mingi kutokana na chuki pamoja na vita; hali ya kutoelewana pamoja na ukosefu wa amani. Katika mtazamo huu, Baba Mtakatifu anakaza kusema,katika maadhimisho haya Bangui na nchi nzima ya Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati wanawakilisha mataifa yote yanayoendelea kubeba Msalaba wa vita na machafuko ya kijamii sehemu mbali mbali za dunia. Bangui kwa sasa ni mji mkuu wa sala ili kuomba huruma ya Mungu, upatanisho, haki, amani, msamaha na mapendo ya dhati kwa jirani. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuomba amani na upendo.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake amekazia umuhimu wa kuvuka ya kale na kuanza kujikita katika maisha mapya; changamoto ya upendo kwa adui na kwamba, Mwenyezi Mungu ana nguvu na upendo wake hauna kifani! Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amemwongoza hadi kufika katika Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kuzindua rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. Hiki ni kipindi ambacho kuna watu ambao wamekata tamaa na wala haana nguvu tena ya kutenda jambo lolote, wanakaa huku wakisubiri kuonwa ili kuonjeshwa wema. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuangalia nguvu ya Mungu inayoponya na kumwezesha mwamini kuanza tena kutembea katika njia mpya, jambo la msingi ni kujiaminisha mbele ya Mungu.

Waamini wanapaswa kukumbuka kwamba, wanaposafiri, Yesu yuko pamoja nao anataka kuvuka mto kwenda upande wa pili akiwa ameandamana nao, tayari kuanza maisha mapya! Bila kumtegemea Yesu, Baba Mtakatifu anasema, safari hii ni bure na wala haitapata mafanikio. Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini humo kuhakikisha kwamba wanaondokana na ukabila unaowatenganisha ili kujenga Kanisa, Familia ya Mungu inayowajibika; Kanisa ambalo liko wazi kwa kila mtu; Kanisa linalohudumia kwa upendo na ukarimu; Kanisa linalotaka kujikita katika umoja na mshikamano wa kidugu, ili kugawana hata kile kidogo walicho nacho pamoja na kuendelea kutumainia na kushuhudia huruma ya Mungu katika maisha.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, wanaboresha wito wao kwa kuonesha upendo hata kwa adui zao, ili kuondokana na kishawishi cha kutaka kulipizana kisasi na hiki ndicho chanzo cha maafa yasiyokoma. Mihimili ya Uinjilishaji inapaswa kuwa ni wajenzi na vyombo vya msamaha, upatanisho na huruma. Kwa njia hii, wataweza kuwasaidia ndugu zao kuvuka mto kuelekea upande wa pili, kwa kuwashirikisha siri, matumaini na furaha inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye anaendelea kusafiri pamoja na waja wake.

Baba Mtakatifu anawahamasisha waamini kutafakari mambao ambayo yanaweza kuwa kwao ni alama makini ya rejea. Jambo la kwanza ni haki, mwaliko kwa kuwa wajenzi wa haki inayojikita katika amani. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa mapendo, kumbe, waamini wanatakiwa kushuhudia haki inayofumbata upendo. Hata katika machafuko na kinzani katika maisha ya mwanadamu anakaza kusema Baba Mtakatifu, Yesu Kristo anataka kuonesha nguvu ya upendo wake, kwani Mungu ana nguvu zaidi kuliko mambo mengine yote!

Baba Mtakatifu amehitimisha mahubiri yake kwa kuwataka wale wote wanaotumia vibaya silaha za dunia hii, kuweka chini silaha hizi za kifo na badala yake wajivike silaha ya haki, upendo na huruma; mambo msingi yanayoweza kukuza na kuimarisha amani. Kwa familia ya Mungu nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Baba Mtakatifu anawataka kumwilisha moyo wa Mungu kati ya ndugu zao. Mavazi ya misa yaliyotumiwa na Baba Mtakatifu katika Ibada ya kuzindua Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na Kalisi yamebaki Jimbo kuu la Bangui kama zawadi kutoka kwa Baba Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.