2015-11-30 12:01:00

Kanisa liwe karibu zaidi na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii


Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1985 alitembelea Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kwa kuwashukuru Wamissionari waliopandikiza mbegu ya Ukristo ambayo kwa wakati huo ilikuwa inaanza kuzaa matunda mengi kwa kuwa na ongezeko kubwa la waamini na miito mitakatifu ya maisha ya Kipadre na Kitawa. Uwepo wake miongoni mwa wananchi wa Afrika ya Kati ilikuwa ni alama ya faraja, matumaini na changamoto ya kujikita katika Injili ya amani kwa kudumisha uhuru, imani, udugu na hali ya kuheshimiana, kila mtu akipewa nafasi ya kuchangia katika ustawi na maendeleo ya nchi yake.

Mtakatifu Yohane Paulo II alikazia pia umuhimu wa upendo kwa jirani unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha, kama kielelezo cha imani tendaji na Injili  inayopewa kipaumbele cha pekee katika sera, mikakati na maisha ya watu. Mama Kanisa anapaswa kuwa karibu zaidi na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa njia ya elimu makini, huduma katika sekta ya afya na maendeleo endelevu. Kanisa lisaidie mapambano dhidi ya ulevi wa kupindukia usiokuwa na tija wala mashiko; liwe mstari wa mbele katika lulinda na kutunza mazingira pamoja na haki msingi za binadamu.

Wananchi watambue kwamba, haki daima inaambatana na wajibu wanaopaswa kuutekeleza kwa dhati, washikamane kulinda na kudumisha mafao ya wengi na kwamba, Wakristo wawe mstari wa mbele katika maboresho ya maisha ya kijamii na kiuchumi kwa kujikita katika misingi ya: majadiliano katika ukweli na uwazi; haki na usawa. Kanisa liendelee kuwekeza miongoni mwa vijana wa kizazi kipya kwa njia ya elimu makini ili kuwajengea matumaini badala ya kuwashutumu kutokana na mapungufu yanayojionesha katika maisha yao ya ujana!

Kanisa liendelee kutoa elimu ya dini shuleni pamoja na kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kweli familia ziweze kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Mtakatifu Yohane Paulo II aliliombea Kanisa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kuwa ni kielelezo na rejea kwa maskini; mahali pa ukweli, uhuru, haki na amani; mahali ambapo upendo unamwilishwa katika huduma makini kwa watu; kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kikanisa pamoja na imani thabiti kwa Kristo Yesu. Kamwe wasikate tamaa, bali wawe na ujasiri wa kusimama tena na kuendelea na safari licha ya magumu na changamoto wanazokabiliana nazo!

Mtakatifu Yohane Paulo II alikaza kusema, Kanisa litaendelea kuwakumbuka daima na kwamba, anawatakia mwanzo mpya unaojikita katika uhuru na ushirikiano, kwa ajili ya kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili wananchi wote waweze kupata furaha ya kweli. Rasilimali na utajiri wa nchi viwe ni kwa ajili ya wote na wala si kwa wajanja wachache. Wakristo waendelee kuchangia kwa hali na mali katika ustawi na maendeleo ya nchi yao. Papa Yohane Paulo II aliwaombea haki na amani, changamoto ambayo bado wanapaswa kuifanyia kazi kwa dhati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.