2015-11-30 15:48:00

Amekuja na ameonekana na wote! Matendo makuu ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 30 Novemba 2015 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa michezo wa Barthèlèmy Boganda ulioko Bangui; Ibada ambayo imehudhuriwa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wakishangilia na kusema, amekuja na ameonekana na wote. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa kujenga Jumuiya inayojikita katika tunu msingi za maisha; waamini wawe na ujasiri wa kuanza safari mpya ya maisha na kwamba, kwa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu wanaanza ukurasa mpya.

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee kabisa anapenda kuungana na Familia ya Mungu Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kumshukuru Mungu kwa zawadi ya imani na matunda yake ambayo ni furaha, mshikamano na upendo ambao bado unakabiliwa na changamoto ambazo zinasababisha mateso katika maisha ya watu: kiroho na kimwili kutokana na mtukio mbali mbali yaliyojitokeza nchini mao.

Wakati hali ya maisha ni tete, kuna majaribu na mahangaiko; watu wanakata tamaa na kuchoka kwa kudhani kwamba, hawawezi tena kufanya jambo lolote. Lakini kwa kumzunguka Kristo katika maadhimisho ya  Fumbo la Ekaristi takatifu, watu wanafurahia tena uwepo na kuonja cheche za maisha mapya na wokovu unaoletwa naye pale wanapovuka kwenda upande wa pili wa mto! Lakini waamini wanakumbushwa kwamba, bado wako safarini na hawajafaulu kuvuka kwenda upande wa pili wa mto! Hapa wanapaswa kufanya maamuzi magumu na yenye ujasiri kwa kujipyaisha katika ari na mwamko wa kimissionari ili kuvuka mto!

Kila mwamini anapaswa kuuvua utu wa kale unaofumbatwa na dhambi; kwa kumkataa Shetani anayeendelea kutenda kazi katika nyakati hizi za machafuko ya kijamii, vita na chuki; mambo yanayowapeleka watu katika ubinafsi na hali ya mtu kujitafuta mwenyewe; dharau, vita, mahangamizi; vitendo vya kulipizana kisasi; kujikatia tamaa pamoja na kuwanyonya maskini na wanyonge.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Jumuiya za Kikristo zinahamasishwa kufuata njia ya utakatifu wa maisha ambayo bado ni ndefu. Waamini wanapaswa kuomba msamaha kwa dhambi na ukakasi katika kushuhudia Injili. Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu ambao umezinduliwa nchini humu, iwe ni fursa kwa wananchi wa Afrika ya Kati kufanya maamuzi magumu ya kuanza ukurasa mpya wa historia ya maisha ya Kikristo, kwa kuwa na mwelekeo mpya, ili kwenda mbali zaidi kwenye kina kirefu! Kila mwamini anahamasishwa kuwa mdumifu katika imani kwa kuendeleza dhamana na utume wa Kimissionari; wawe ni wajenzi wa upyaisho wa maisha ya kiutu na kiroho nchini mwao!

Mara baada ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi, Baba Mtakatifu amemkumbuka kwa namna ya pekee Patriaki Bartolomeo wa kwanza, Kanisa linapoadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume na kumtakia matashi mema; furaha na udugu. Anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuyabariki Makanisa haya mawili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.