2015-11-29 17:16:00

Ondoeni: Ukabila, udini, itikadi na matabaka ili kujenga amani na utulivu!


Wakimbizi na wahamiaji ni kati ya watu ambao wanaendelea kupata upendeleo wa pekee katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Jumapili tarehe 29 Novemba 2015 mara baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na viongozi wa Serikali, wanasiasa na wanadiplomasia, Baba Mtakatifu alikwenda moja kwa moja kutembelea kambi ya wakimbizi ya Mtakatifu Sauveur iliyoko mjini Bangui. Hapo amekutana na wakimbizi na kuwapatia neno la faraja.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amewatakia wote amani, msamaha, umoja na mshikamano wa kitaifa; mambo ambayo watoto waliompokea wakati alipowasili kambini hapo waliyaandika kwenye mabango yao. Baba Mtakatifu anawahamasisha wananchi na watu wote wenye mapenzi mema kujisadaka kwa ajili ya kudumisha misingi ya amani inayojikita katika upendo, urafiki, maridhiano na msamaha wa kweli. Pasi na mambo haya muhimu katika maisha, amani itaendelea kuwa ndoto kwa wengi anasema Baba Mtakatifu.

Hapa kila mtu anapaswa kuchangia ili kweli amani iweze kupatikana! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba wananchi wa Afrika ya Kati wataweza kuanza mchakato wa amani kwa kushikamana na kuondokana na mambo ambayo yanawatenga na kuwagawanya kwa misingi ya ukabila, udini, itikadi na tabaka la mtu katika jamii. Watu wote wanapaswa kuambata amani kwani ni ndugu wamoja na wanaotamani kuona amani ya kweli ikitawala midomoni na mioyoni mwao. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewapatia baraka zake za kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.