2015-11-28 17:56:00

Vijana msikubali kumezwa na malimwengu!


Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi jioni tarehe 28 Novemba 2015 amekutana na umati wa vijana waliokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa ndege Kololo, Jijini Kampala, Uganda. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia mambo makuu matatu: matumaini ya Kikristo; vijana kamwe wasikate tamaa wanapokutana na matope katika maisha na wasiogope kuwa tofauti na wengine ili kutomezwa na malimwengu. Baba Mtakatifu anasema matumaini ya Kikristo yanajikita katika ahadi ambazo Yesu Kristo amewaachia wafuasi wake na kwamba, ahadi hizi zinafumbatwa katika nguvu ya upendo.

Vijana wanapokumbana na vikwazo pamoja na vizingiti katika maisha na kujisikia kukata tamaa, wajitahidi kujishikamanisha na upendo wa Kristo ambao una nguvu ya kuweza kubadili kifo kuwa chemchemi ya maisha mapya kiasi cha kufukuza mabaya yote katika maisha. Baba Mtakatifu anakiri kwa kusema kwamba, jambo hili si rahisi sana katika maisha ya vijana kwani kuna umati mkubwa wa watu waliokata na kujikatia tamaa.

Vijana watambue kwamba, katika safari ya maisha yao wanaweza kutumbukia katika matope kiasi cha kuwakatisha tamaa. Matope haya anasema Baba Mtakatifu ni umaskini, ukosefu wa fursa mbali mbali na hata wakati mwingine kukosa mafanikio katika maisha na hivyo kujikuta wakitumbukia katika hali ya kukata tamaa. Vijana wawe tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kama vile ambavyo mtoto mdogo anapoona kwamba, hana nguvu tena anakimbilia huruma ya baba yake mzazi. Vijana wajifunze kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kwani Yeye yuko pamoja nao daima.

Baba Mtakatifu anawahimiza vijana wasiogope kupenda na kupendwa ili kujenga na kudumisha familia inayojikita katika upendo wa dhati kati ya bwana na bibi ili kutangaza na kushuhudia Injili ya familia kadiri ya mafundisho ya Kanisa. Vijana wasipokubali kujaribu na kupima nguvu zao, watakabaki wakiwa wameshangaa pasi na kufanya maamuzi magumu katika maisha.

Baba Mtakatifu anawahamasisha vijana kutoogopa kamwe kuwa tofauti na vijana wengine wanaofuata mikumbo ya maisha, bali wawe na ujasiri wa kusema hapana na kukataa kumezwa na malimwengu! Vijana wajifunze kuwa na mwelekeo tofauti hata kama unasigana na mawazo ya vijana wengi kwa kuambata kanuni maadili, mila na desturi njema za Kiafrika. Mashahidi wa Uganda wawe ni mfano bora wa kuigwa, tayari kushuhudia mwanga wa imani uking’aa katika maisha ya familia zao, shuleni na katika maeneo ya kazi. Vijana wawe na ujasiri wa kuanzisha mchakato wa majadiliano ya wengine kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.