2015-11-28 10:19:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio


Mpendwa mwana wa Mungu, Mama Kanisa kama kawaida akiongozwa na Roho Mtakatifu, daima haachi kutuwekea vipindi kwa ajili ya kujitakatifuza na kuongoza maisha yetu tukimwelekea Mungu zaidi na zaidi. Tunamshukuru Mungu kwa upendo wake anaotujalia kwa njia ya Kanisa. Tulimaliza mwaka wa Kanisa vizuri Dominika iliyopita na sasa tunaanza mwaka mpya wa Kanisa yaani mwaka C. Kumbe, leo ni Dominika ya kwanza Kipindi cha Majilio, Dominika ambayo hufungua mwaka mpya wa Kanisa. Ni Dominika ambayo hufungua kipindi cha Dominika 4 kwa ajili ya matayarisho ya ujio wa Masiha Mkombozi yaani kuzaliwa Mtoto Emanueli aliye Mwana wa Mungu.

Katika Dominika hii ya kwanza ya Majilio na zaidi kipindi chote cha Majilio ujumbe wa Neno la Mungu ni kuhusu kutayarisha njia ya Bwana. Tutakutana na Nabii Yeremia ambaye mafundisho yake yanakazia timizo la ahadi za Mungu alizoweka kwa Wana wa Israeli. Ahadi yenyewe ni ile yakwamba atawapelekea mfalme ambaye atazaliwa katika kiti cha Daudi. Mungu hatoi ahadi tu ya kuwapelekea mfalme bali mfalme huyu atakuwa mfalme wa haki na amani, atawatawala kwa unyofu wa hali ya juu. Ahadi hii ya Mungu inatimia anapozaliwa Yesu Kristo Masiha katika ukoo wa Daudi.

Mpendwa unayenisikiliza, dhamira kuu ya majilio ni matayarisho kwa ajili ya kumpokea Mkombozi, kumbe matayarisho hayo yanajikita katika kujiweka tayari kiroho na kwa namna hiyo dhihirisho likiwa matendo mema daima katika jumuiya zetu. Matayarisho ni kutenda mapenzi ya Mungu, ni kupendana na kuheshimiana na kuishi kidugu. Matayarisho kadiri ya Mwinjili Luka ni pia kuacha mambo ya zamani na kuishi maisha mapya. Kielelezo cha maisha ya zamani ni ulevi, anasa na shughuli nyingine za kidunia zisizojenga ufalme wa Mungu. Kwa kuacha maisha ya zamani tunajiweka tayari ili Bwana ajapo atukute tu tayari kwa kunyakuliwa naye.

Ewe ndugu yangu unayenisikiliza silaha ambayo Mwinjili anatupatia ni maisha ya SALA. Sala ni maongezi na Mungu na hivi kila asaliye hukaa karibu na babaye na kwa jinsi hiyo ajapo hawezi kukuta hayuko tayari. Mtume Paulo anapowaandikia Wathesalonike anawaasa kujiunda katika fadhila ya kupendana kati yao na kwa njia hii watakuwa tayari kumlaki Bwana wakati ajapo kuwahukumu wazima na wafu!

Mpendwa mwana wa Mungu, mafundisho haya ni kwa ajili yetu hivi leo, yaani tunapaswa kujenga familia iliyosimama katika msingi wa maelewano na mapendo kina. Kipindi cha majilio ni kipindi cha kupanda mbegu bora ya uaminifu, utii, matumaini ili mwishoni tuvune tunda moja zuri nalo ni kupokea mwanga wa milele, yaani uzima wa milele. Majilio yatudai kupokea sakramenti, kushiriki Misa takatifu, kuwatembelea wagonjwa, kukesha katika sala na mambo yote mazuri yanayokusudia kusimika ufalme wa Mungu.

Nikutakie maisha na majilio njema na kipindi chema cha Noeli na Mwaka mpya 2016, Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.