2015-11-28 08:45:00

Matunda ya mashuhuda wa imani yanajionesha nchini Uganda!


Askofu mkuu Cyprian Kizito Lwanga wa Jimbo kuu la Kampala, Uganda mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 28 Novemba 2015 kama kilele cha Jubilei ya miaka 50 tangu  Mashahidi wa Uganda walipotangazwa kuwa watakatifu hapo tarehe 18 Oktoba 1964 amesema, Namgongo ni mahali ambapo mashuhuda wa imani kutoka Uganda waliyamimina maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake, hija ya mateso iliyoanzia Munyonyo na kuhitimishwa hapo tarehe 3 Juni 1886. Hili ni eneo ambalo limebahatika kutembelewa na Mwenyeheri Paulo VI na Mtakatifu Yohane Paulo II.

Mashuhuda wa imani nchini Uganda wamekuwa kweli ni chemchemi ya miito mitakatifu ya Upadre na Utawa, kwani imeongezeka maradufu nchini Uganda. Ibada kwa Mashahidi wa Uganda imeenea sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, kuna: Makanisa na taasisi ambazo zimewateua Mashahidi wa Uganda kuwa wasimamizi wao pamoja na kuongezeka kwa utume wa wamini walei nchini Uganda. Mashuhuda wa imani wamefungua kurasa mpya za maisha na utume wa Kanisa nchini Uganda na Afrika katika ujumla wake. 

Afrika inasimama na imekombolewa kwa damu ya mashuhuda wa imani kiasi kwamba kwa sasa Bara la Afrika limekuwa ni nyumba ya Injili na maskani mapya ya Yesu. Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda linaishukuru Serikali kwa kuamua kwamba, tarehe 3 Juni ya kila mwaka kuwa ni Siku ya Mapumziko ili kuwaenzi Mashahidi wa Uganda, tayari kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha yao ya kila siku.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.