2015-11-27 07:47:00

Watawa wako mstari wa mbele katika huduma kwa Familia ya Mungu nchini Kenya


Wakleri, Watawa na Majandokasisi  kutoka Kenya, Alhamisi tarehe 26 Novemba 2015 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Wamemshirikisha ushuhuda wa maisha na utume wao kwa Familia ya Mungu nchini Kenya katika medani mbali mbali za maisha. Monsinyo Anthony Ireri Mukobo, Mwenyekiti wa Tume ya Wakleri na Watawa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya amemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Tume hii inapania pamoja na mambo mengine kujenga na kuimarisha mahusiano mema kati ya Maaskofu, Wakleri na Watawa, ili kutekeleza dhamana ya kinabii na kiinjili kwa ajili ya Familia ya Mungu nchini Kenya.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuitisha maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani ili waweze kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa nchini Kenya imekuwa ni fursa ya kufanya tafakari ya kina kuhusu maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linashirikiana  kwa karibu sana na Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Kenya pamoja na Chuo kikuu cha Tangaza, kilichoko nchini Kenya.

Monsinyo Mukobo anakaza kusema, watawa wamekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa Familia ya Mungu nchini Kenya hususan katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, huku wakijisadaka bila ya kujibakiza, kiasi hata cha kuyamimina maisha yao wakiwa katika huduma kama ilivyotokea kwa Mwenyeheri Sr. Irene Stephani Nyaatha aliyetangazwa hivi karibuni na Mama Kanisa kuwa ni Mwenyeheri. Wakleri na Watawa wanamshukuru Baba Mtakatifu kwa kuendelea kuhimiza utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kulinda utu na heshima ya watoto, ili kuendelea kuwa kweli ni Injili hai kati ya watu!

Kwa upande wake Sr. Michael Marie Rottinghous, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kwa Watawa wa Kike Kenya, AOSK,  ameonesha ustawi na ukuaji wa mashirika ya kitawa nchini Kenya; kwa kuendelea kutunza utambulisho wao katika ulimwengu wa utandawazi; kwa kukazia malezi na majiundo endelevu kwa watawa na wanovisi tayari kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu katika huduma na ushuhuda; kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Uhai, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza.

Naye Padre Felix J. Phiri, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Kenya, RSCK ametumia nafasi hii kumshukuru Baba Mtakatifu kwa kutangaza Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani na kwamba, wamekuwa mstari wa mbele kutafakari: historia, maisha na utume wao ndani ya Kanisa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali. Watawa wako mstari wa mbele katika kulinda na kutunza mazingira; kwa kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa nchini Kenya; kulinda na kuwatetea watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.