2015-11-27 16:33:00

Vijana wanakerwa na rushwa, ukabila na ugaidi! Papa Francisko atoa somo!


Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 27 Novemba 2015 amekutana na kuzungumza na vijana kutoka sehemu mbali mbali za Kenya kwa kujibu maswali makuu matatu yaliyokuwa yanawakera sana mioyoni mwao. Swali la kwanza liligusia saratani ya rushwa Barani Afrika; ukabila unaoendelea kunyanyasa na kudhohofisha umoja na mafungamano ya kijamii bila kusahau vitendo vya uvunjifu wa haki na amani; mambo ambayo yanaonekana kuwa na mvuto kwa vijana wanaotafuta njia ya mkato katika maisha!

Baba Mtakatifu amewashukuru vijana waliosali kwa ajili ya kuombea hija yake ya kitume Barani Afrika kwa kusema kwamba, mtu ambaye ni mkavu katika maisha ya sala anapoteza utu wake kwani mtu wa namna hiyo anajikuta akiwa na kiburi kiasi hata cha kumsahau Mungu katika maisha yake. Maisha yana changamoto nyingi, kumbe kuna haja ya kuendelea kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi wa maisha ya mtu binafsi, familia, jamii na ulimwengu katika ujumla wake. Watu wanaishi katika ulimwengu ambamo kuna raha, shida na changamoto zake, hivyo wanapaswa kumwomba Mungu awajalie neema ya kushinda magumu katika maisha yao!

Baba Mtakatifu amegusia ukabila unaovuruga umoja na mshikamano wa kitaifa na kwamba, watu wanaweza kushinda ukabila kwa kusikilizana na kusaidiana katika mambo mbali mbali ya maisha. Huu ni mchakato wa kudumisha majadiliano katika tamaduni ili kujenga na kudumisha moyo wa sala na upatanisho, wote wakiwa wameshimana katika umoja na udugu. Mapambano dhidi ya ukabila ni mchakato endelevu wa kufungua miyo kwa ajili ya wengine.

Baba Mtakatifu amejikita katika saratani ya rushwa na madhara yake katika jamii nyingi duniani, kwani ni kama sukari tamu, lakini inasababisha madhara makubwa. Rushwa ni ugonjwa ambao umeenea sehemu mbali mbali za maisha ya binadamu: kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata wakati mwingine kidini, bila kusahau kwamba hata Vatican inaguswa pia na suala la rushwa. Kila mtu anapaswa kuikata rushwa kutoka moyoni na maisha mwake kwani rushwa ni adui wa haki na huduma makini kwa jamii kiasi cha kusababisha mateso kwa watu wasiokuwa na hatia. Rushwa ni safari inayompeleka mla na mtoa rushwa kwenye kifo!

Baba Mtakatifu anawataka wadau mbali mbali kutumia vyema njia za mawasiliano ya kijamii kwa ajili ya kutangaza Injili ya uhai na matumaini kwa wale waliokata tamaa, ili hatimaye, kujenga madaraja ya watu kukutana na kusaidiana kama ndugu. Aanwataka vijana kusali na kusimamia kanuni maadili, kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa makini na kamwe wasitumbukizwe katika misimamo mikali ya kidini, kisiasa na kikabila kwani inavuruga haki, amani na mshikamano wa kitaifa. Wasikubali kutumiwa na wajanja wachache kwa ajili ya kufanya vitendo vya kigaidi, bali watoe kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na wala si uchu wa mali na madaraka mambo ambayo kimsingi ni chanzo cha vita na kinzani nyingi za kijamii.

Baba Mtakatifu anawataka vijana katika shida na mahangaiko yao kumwangalia Kristo Yesu, ufunuo wa Baba mwenye huruma na mapendo kwa waja wake. Fumbo la Msalaba ni alama ya hali ya juu kabisa ya upendo wa Mungu kwa binadamu na chemi chemi ya matumaini. Baba Mtakatifu amewaambia vijana kwamba, mfukoni mwake anatembea daima na Rozari takatifu, muhtasari wa historia ya kazi ya ukombozi na Njia ya Msalaba inayoonesha jinsi Mungu alivyojinyenyekesha kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Baba Mtakatifu anawataka vijana kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Wawe ni faraja kwa wapweke na wote wanaoteseka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.