2015-11-27 16:54:00

Papa Francisko atinga timu Uganda! Mashuhuda wa imani ni mashujaa wa nchi!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuzungumza na Maaskofu Katoliki Kenya, aliondoka kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kuelekea Entebe, Uganda ambako amewasili jioni na kupoklewa na mwenyeji wake Rais Yoweri kaguta Museveni wa Uganda kwa heshima zote za kitaifa. Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa viongozi wa Serikali ya Uganda, Wanasiasa na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao, amegusia mambo makuu matatu: mashahidi wa Uganda kuwa kweli ni mashujaa wa kitaifa; umuhimu wa Bara la Afrika katika medani za kimataifa pamoja na kuishukuru Uganda kwa kutoa hifadhi kwa wakimbizi.

Baba Mtakatifu anasema lengo lake la kwanza katika hija yake Barani Afrika ni kutoa heshima kwa mashuhuda wa imani walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa na kutangazwa watakatifu, miaka 50 iliyopita. Wao ni alama ya urafiki na chachu inayowatia moyo wananchi wa Uganda kujikita katika mambo muhimu katika maisha. Mashahidi wa Uganda wametoa maisha yao kwa ajili ya Mungu, hata katika tofauti zao, wameonesha umoja changamoto ya wananchi wa Uganda kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wanaojenga familia moja ya binadamu.

Baba Mtakatifu anawawataka viongozi wa Bara la Afrika kuhakikisha kwamba wanafumbata kanuni hizi katika utekelezaji wa sera na mikakati yao ya uongozi, kwa kuwa wakweli na wawazi; kwa kudumisha utawala bora; maendeleo endelevu pamoja na ushiriki wa watu wote katika ujenzi wa nchi yao bila kusahau kuwa na mgawanyo bora wa rasilimali za nchi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hija yake ya kichungaji Barani Afrika inalenga kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Bara la Afrika na watu wake. Kuaamsha ari na moyo wa kusonga mbele katika mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi; kuendeleza matumaini na changamoto kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika. Hii ni changamoto kubwa ya kuhakikisha kwamba, raslimali ya nchi husuan nguvu kazi na rasilimali watu inatumika barabara ili kujenga na kuimarisha misingi bora ya maisha ya kifamilia.

Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Bara la Afrika kulinda na kutunza vyema  maliasili ya Afrika ili kuwasaidia vijana kupata elimu na fursa za ajira ili hatimaye, waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa nchi yao. Baba Mtakatifu anaishukuru Uganda kwa namna ya pekee kwa kutoa hifadhi kwa wakimbizi kielelezo cha ukarimu wa wananchi wa Uganda hata katika umaskini wao. Huu ni mfano bora wa kuigwa kwa mataifa mengine. Dunia imegubikwa na vita, kinzani na ukosefu wa haki msingi za binadamu pamoja na wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi ambalo halijawahi kutokea tangu. Haya ni matukio ambayo yanapima umakini wa binadamu mamboleo; utu na heshima ya binadamu, upendo na mshikamano wa dhati kwa kusaidiana kama ndugu wamoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.