2015-11-27 07:06:00

Jitoseni kimasomaso kwa ajili ya huduma kwa Mungu na maskini!


Mwenyezi Mungu amewachagua watu wake kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo inayowapatia baadhi nafasi ya kumtumikia kwa karibu zaidi kwa njia ya Daraja Takatifu na Maisha ya wakfu hapa hakuna njia ya mkato, kila mtu anapaswa kuingia kwa kutumia mlango mkubwa! Hakuna cha rushwa wala kitu kidogo, kama kuna mtu ambaye anataka kumtumikia Mungu kwa njia za panya, hapa si mahali pake, anaweza kumtumikia Mungu katika maisha mengine na wala si katika Daraja Takatifu au Utawa. Ikumbukwe kwamba, Yesu Kristo ndiye njia na mlango wa maisha ya uzima wa milele. 

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 26 Novemba 2015 wakati alipokutana na kuzungumza na Wakleri, Watawa na Majandokasisi kutoka Kenya wakati wa hija yake ya kitume nchini Kenya. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwenyezi Mungu amewachagua, akawalea na kuwafunda na anataka kuwatuma ili kuwa ni wahudumu wa Injili ya Kristo, matendo makuu ya Mungu anayewaangalia waja wake kwa jicho la upendo.

Kuna baadhi ya watu wanajisikia kuwa wana wito lakini hawana uhakika wa maisha na utume wao, Baba Mtakatifu anasema, wasikate tamaa kwani hata miongoni mwa Mitume wa Yesu, kuna baadhi hawakufahamu undani wa wito wao wakatamani malimwengu na upendeleo kutoka kwa Yesu ili waweze kukaa mkono wake wa kulia na mwingine wa kushoto! Hiki ni kishawishi cha kutaka kumfuasa Kristo kwa tamaa ya fedha na madaraka; mambo ambayo yanajionesha taratibu na hatimaye kukomaa katika maisha ya mtu! Ufuasi wa Kristo unakinzana kabisa na tamaa ya madaraka na uchu wa mali, kwa ni mtu anayetaka kumfuasa Kristo anapaswa kuangalia utukufu wa Fumbo la Msalaba. Kanisa anasema Baba Mtakatifu ni Fumbo linalowaalika waamini kumwangalia na kumfuasa Kristo kwa ari na moyo mkuu. Wakleri na watawa watambue kwamba, kwa kuitwa na Yesu hawaondolei mapungufu yao ya kibinadamu  la hasha! Wataendelea kuwa wadhambi wanaohitaji kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu.

Mwenyezi Mungu aliyeanzisha kazi njema mioyoni mwa waja wake ataikamilisha kwa wakati wake anasema Baba Mtakatifu Francisko. Mbegu ya wito inashughulikiwa na watu mbali mbali hadi kuzaa matunda ya Upadre na Utawa. Katika shida na mahangaiko ya ndani, Wakleri na Watawa wasisite kumlilia Mwenyezi Mungu kwani kuna Mitume waliangua kilio kwa kumsaliti Yesu kwa kutambua kwamba, wao ni wadhambi. Kwa mtawa ambaye macho yake ni makavu na ameacha kulia, hapa kuna jambo ambalo si sawa! Wakleri na Watawa waendelee kumlilia Mungu kwa kukosa uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake; kwa ajili ya mateso na mahangaiko ya dunia; wawalilie wazee na watoto wanaotelekezwa na kuuwawa kikatili; walie hata kwa yale mambo ambayo bado yanaendelea kuwa ni mafumbo katika maisha yao.

Baba Mtakatifu amekaza kusema, Fumbo la Mateso na mahangaiko ya mwanadamu halina jibu la moja kwa moja hapa duniani. Kuna watoto ambao wanateseka kwa kuandamwa na saratani, mwaliko wa kumwangalia Kristo Msalabani, jibu makini kwa ukosefu wa haki msingi za binadamu, mateso na mahangaiko ya watu. Lakini baada ya mateso na kifo, siku ya tatu Yesu alifufuka kwa wafu! Mateso ya Yesu yawakumbushe Wakleri na Watawa kwamba, wanaweza hata wao kutumbukia katika dhambi hivyo kumchukiza Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anawataka Wakleri na Watawa kuwa karibu zaidi na Yesu kwa njia ya sala, kwani watakapokumbwa na kishawishi cha kutosali hapo watanyauka na kukauka kama jani la mgomba! Wajitahidi kutenga muda wa kutosha kwa ajili ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, mambo ambayo yanamsaidia  Padre au Mtawa kuwa karibu zaidi na Yesu. Wawe ni wahudumu mahiri wa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; huduma iwaguse hata wale wenye majivuno na wadhambi na kwamba, wamechaguliwa na Yesu ili kutumikia na wala si kutumikiwa!

Watumikie kwa kujisadaka la wala si kwa kutaka kulipwa fidia na kwamba, Mwenyezi Mungu aliyeianzisha kazi njema ndani mwao ataikamilisha kwa wakati wake. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Wamissionari wote waliojitosa kimasomaso kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, leo hii wamelala katika usingizi wa amani wakiwa na tumaini la ufufuko! Anawapongeza Wakleri na watawa wanaoendelea kutoa huduma zao katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu kwa watu: kiroho na kimwili, lengo ni kuhudumia na wala si kuhudumiwa!

Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake iliyokuwa inabubujika kutoka katika undani wa maisha yake kwa kuwashukuru wote pamoja na kuwatia shime ili waendelee kusonga mbele licha ya dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu; waendelee kuwasaidia wagonjwa kufa kifo chema; wawe kweli ni wahudumu wa Injili ya matumaini katika maisha, wajitahidi daima kuwa ni watu wa msamaha.

Baba Mtakatifu amewakumbusha Majandokasisi kwamba, hata kama hakuwataja moja kwa moja, lakini watambue kwamba, wao pia wanaguswa na ushauri alioutoa kwa Wakleri na Watawa. Ikiwa kama kuna jandokasisi anajisikia kwamba, huu si wito wake, awe na ujasiri wa kuamua mapema, ili aweze kutafuta aina nyingine ya maisha, kwa kuoa ili kuunda familia! Baba Mtakatifu alikutana na watoto wagonjwa wa Saratani na kuwafariji na hatimaye akawapatia baraka zake za kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.