2015-11-26 11:50:00

Viongozi wa kidini wanamshukuru Papa kwa kusimama kidete kutetea wanyonge!


Viongozi mbali mbali wa kidini nchini Kenya, Alhamisi tarehe 26 Novemba 2015 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa maridhiano, haki na amani miongoni mwa waamini. Askofu Peter Kairo, mwenyekiti wa Tume ya Majadiliano ya kidini kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya amemwelezea Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Kenya ina waamini wa dini mbali mbali ambao uhuru wao wa kuabudu unatambuliwa Kikatiba. Nchini Kenya kuna Mabaraza ambayo yanawaunganisha waamini wa dini mbali mbali nchini humo ili kuweza kuishi kwa amani, huku wakishirikiana.

Askofu mkuu Eliud Wabukala wa Kanisa Anglikana Kenya amemwambia Baba Mtakatifu kwamba, uwepo wake miongoni mwao ni muhimu sana katika mchakato wa kudumisha majadiliano ya kiekumene miongoni mwa wafuasi wa Kristo. Amempongeza kwa Waraka wake wa kitume, juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Laudato si unaowahimiza juu ya matumizi bora ya raslimali ya dunia kwa ajili ya kizazi cha sasa na kile kijacho sanjari na matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira.

Askofu mkuu Wabukala amekazia kuhusu utakatifu wa maisha unaotishiwa na utamaduni wa kifo. Ujio wa Baba Mtakatifu Barani Afrika uwe ni changamoto kwa Familia ya Mungu kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai pamoja na tunu msingi za Kiinjili pamoja na kuendeleza mshikamano kati ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Anawaalika waamini kuonesha upendo kwa Kristo Yesu na kumtolea ushuhuda Yeye ambaye ni mwanga na matumaini ya watu.

Viongozi wa kidini nchini Kenya wanataka kuendelea kushikamana katika kulinda na kudumisha amani na utulivu kati ya watu. Kenya kama zilivyo nchi nyingine za Kiafrika katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni imeendelea kucharuka katika medani mbali mbali za maisha, lakini pengo kati ya maskini na matajiri linazidi kuongezeka kwa kasi ya ajabu, changamoto kubwa ili kuhakikisha kwamba, rasilimali na utajiri wa nchi vinatumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Walimwengu watambue kwamba, wanategemeana na kukamilishana, mwaliko kwa watu wote wenye mapenzi mema kuwa waaminifu kwa kuwajibika pamoja na kujikita katika kanuni maadili, utu wema na imani ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Kwa upande wake Professa Abdulghafur H. S. El Busaidy, rais wa Baraza kuu la Waislam Kenya, SUPKEM ameelezea dhamana na wajibu wa chombo hiki muhimu kwa waamini wa dini ya Kiislam wanaounda asilimia 30% ya idadi yote ya wananchi wa Kenya. Anasema kama viongozi wa kidini wanalo jukumu la kuhakikisha kwamba wanakuza na kudumisha haki, upendo, ukweli, uaminifu na matumani dhidi ya ukosefu wa misingi ya haki, chuki, uchoyo pamboja na mambo yote yanayosababisha kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema. Waamini wa dini mbali mbali watambue kwamba, wote ni watoto wa Mwenyezi Mungu na wakazi wa dunia hii, lakini kwa bahati mbaya dunia inaendelea kujikuta ikiogelea katika vita, chuki na uhasama. Watu wengi wamekengeuka kwa kukosa maadili; kwa kuwa na uchu wa mali na madaraka hata pasi na kufanya kazi; pamoja na kupenda njia za mkato katika maisha mambo ambayo ni hatari kwa maendeleo ya watu.

Baraza kuu la Waislam nchini Kenya linampongeza Baba Mtakatifu kwa Waraka wake wa kitume juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Waamini wa dini ya Kiislam wanataka kushirikiana na waamini wa dini mbali mbali nchini Kenya ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Amani kati ya waamini ni muhimu sana katika kukoleza amani duniani. Juhudi hizi hazina budi kujikita katika majadiliano ya kidini sanjari na kanuni maadili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.