2015-11-26 10:37:00

Viongozi wa kidini wakuze majadiliano, wawe ni vyombo vya amani wakatae udini!


Baba Mtakatifu Francisko ameianza siku ya pili ya hija yake ya kitume Barani Afrika, 26 Novemba 2015 kwa kukutana na kuzungumza na viongozi wa kidini nchini Kenya. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia umuhimu wa majadiliano ya kidini na kwamba, hii ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu pia amewataka viongozi wa kidini kushikamana kwa dhati katika mapambano dhidi ya misimamo mikali ya kidini inayofumbata wakati mwingine vitendo vya kigaidi, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa Katoliki linathamini na kuenzi imani za dini nyingine kama sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha urafiki na kwamba, mahadiliano ya kidini na kiekumene ni jambo muhimu sana katika kuganga na kuponya majeraha ya kinzani, vita na mipasuko ya kijamii. Ushuhuda wa imani tendaji na mshikamano wa dhati ni chemchemi ya mwanga, hekima na mshikamano katika maisha ya kijamii.

Viongozi wa kidini wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanasaidia kuwafunda waamini na jumuiya zao ili ziweze kukua bila kusahau kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ukweli na tunu msingi za maisha kutoka kwa wahenga wao, ili hatimaye ziweze kukita mizizi katika akili na mioyo ya watu, alama ya baraka kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Katika jamii inayojipambanua katika demokrasia na tofauti za watu kama ilivyo kwa Kenya, ushirikiano na umoja miongoni mwa viongozi wa dini mbali mbali ni jambo muhimu sana kwa ajili ya mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kutokana na mwelekeo huu kuna haja kwa waamini wa dini mbali mbali kujitaabisha kufahamiana, ili kujenga na kudumisha urafiki na ushirikiano, tayari kusimama kidete kulinda na kutetea utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Watu wana haki ya kuishi katika uhuru na furaha ya kweli. Ili kufikia lengo hili dini hazina budi kutekeleza dhamana nyeti ya kuwajengea watu dhamiri nyofu; kuwafunda vijana wa kizazi kipya katika tunu msingi za maisha ya kiroho na kitamaduni, ili kuwaandaa kuwa kweli ni raia wema wanaoweza kushuhudia ukweli, ukamilifu pamoja na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu badala kuwa na uchu wa mali na madaraka.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika viongozi wa dini nchini Kenya kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni vyombo vya huduma kwa Mwenyezi Mungu asili ya amani; ambaye jina lake ni takatifu na kamwe halipaswi kutumiwa vibaya kwa kupandikiza mbegu ya chuki, uhasama na mauaji kama ilivyojitokeza kwenye mauaji ya kigaidi ya Westgate Mall, Chuo Kikuu cha Garissa na Mandera. Kwa bahati mbaya, vijana wanatumbukizwa kwenye misimamo mikali ya kidini na wajanja wachache ili kupandikiza mbegu ya chuki, uhasama, woga na wasi wasi ili kuharibu msingi wa mafungamano ya kijamii.

Viongozi wa kidini wanapaswa kutambuliwa kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani, wanaowaalika watu wengine kuishi katika misingi ya haki, amani na utulivu kwa kuheshimiana. Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kugusa mioyo ya watu wanaoendelea kusababisha mauaji ili kuacha matendo yao na kuanza kuambata amani kwa ajili ya familia na jamii katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa Katoliki linaadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipohitimisha maadhimisho ya Mtaguso uliotoa dira na mwongozo kwa Kanisa kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kuwasaidia watu kufahamiana pamoja na kudumisha urafiki. Baba Mtakatifu anasema msimamo huu unapata chimbuko lake katika upendo wa Mungu na wokovu unaotolewa kwa wote.

Walimwengu wanapenda kuona waamini wa dini mbali mbali wakishirikiana kwa dhati na watu wote wenye mapenzi mema ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoiandama familia ya binadamu. Baba Mtakatifu anasema umfika wakati wa watu kuangaliana kama ndugu, wakiwa wameungana katika amani licha ya tofauti zao mbali mbali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.