2015-11-25 11:51:00

Salam na matashi mema kutoka kwa Papa Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kuelekea Barani Afrika amewaandikia ujumbe wa matashi mema Marais wa Italia, Ugikiri, Misri, Sudan na hatimaye, Kenya ambako ameanza hija yake ya kitume Barani Afrika. Baba Mtakatifu katika ujumbe aliomwandikia Rais Prokopis Pavlopoulos wa Ugiriki, amewatakia ustawi na maendeleo wananchi wote wa Ugiriki pamoja na kuwapatia baraka zake za kitume!

Akiwa kwenye anga la Misri, Baba Mtakatifu amemtumia salam za matashi mema Rais Abdel Fattah Sisi wa Misri pamoja na kuwapatia wananchi wote wa Misri baraka zake za kitume, ustawi na amani. Baba Mtakatifu amemwambia Rais Omar Al Bashir wa Sudan Kongwe kwamba, anapoingia kwenye anga la nchi yake, anapenda kuwatakia wananchi wote wa Sudan amani, ustawi na maendeleo. Baba Mtakatifu akiwa kwenye anga la Ethiopia amemtumia salam za matashi mema Rais Mulatu Teshome, kwa kumhakikishia sala na maombezi yake kwa wananchi wote wa Ethiopia.

Baba Mtakatifu Francisko alipoingia kwenye anga la Kenya hata kabla ya kutua kwenye Uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta, amemtakia matashi mema, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya pamoja na wananchi wote wa Kenya ustawi na maendeleo na kwamba, anatarajia kukutana na kuzungumza nao, ili kuwashirikisha furaha na matumaini yake anapotembelea nchini Kenya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.