2015-11-25 16:01:00

Papa kutembelea Tanzania kunako mwaka 2018?


Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican kuhusu hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika kuanzia tarehe 25 – 30 Novemba 2015 kuwa ni kielelezo cha ujasiri wa kinabii. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema Barani Afrika kumsindikiza Baba Mtakatifu katika hija yake Barani Afrika. Kuwa tayari kupokea wosia na changamoto anazotaka kulipatia Kanisa Barani Afrika. Ikumbukwe kwamba, Kenya, Uganda na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati wanawakilisha Familia ya Mungu Barani Afrika.

Askofu mkuu Ruwai’chi anakaza kusema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati ina umuhimu wake wa pekee licha ya changamoto za ulinzi na usalama wa watu na mali zao. Hii ni nchi ambayo imepitia vipindi vigumu vya maisha kijamii kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Watu wameguswa na kutikiswa na misimamo mikali ya kidini kiasi kwamba, wanahitaji kuanza mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kweli; tayari kushikamana katika ujenzi wa umoja wa kitaifa.

Wananchi wa Afrika ya Kati wanaendelea kutumbukia katika janga la umaskini na magonjwa kutokana na vita. Kumbe, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini humo ni kielelezo cha sauti ya kinabii na kwamba kweli ni mjumbe wa haki na amani anayetaka kukoleza mchakato wa upatanisho kati ya watu, tayari kuanza ukurasa mpya wa maisha kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja.

Kanisa Katoliki nchini Tanzania linajiandaa kuadhimisha Jubilei ya miaka 150 ya Ukristo Tanzania Bara, ifikapo mwaka 2018. Hiki kitakuwa ni kipindi cha kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa mafanikio makubwa yaliyokwisha kupatikana nchini Tanzania katika kipindi cha miaka 150 ya uhai wa Kanisa. Kanisa limeenea, linatia matumaini na linaendelea kusonga mbele. Linataka kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwasaidia waamini kuwa kweli ni chachu, chumvi na mwanga wa mataiafa.

Askofu mkuu Ruwa’ichi anakaza kusema, Jubilei ya miaka 150 ya Ukristo nchini Tanzania ingekuwa ni fursa makini ya kumwalika Baba Mtakatifu ili kutembelea Tanzania ili kuwashika mkono watanzania na kuwaimarisha katika imani. Hii ni kazi ambayo inapaswa kutekelezwa na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania pamoja na Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania ili kuangalia uwezekano wa kumwalika Baba Mtakatifu kutembelea Tanzania kunako mwaka 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.