2015-11-25 17:06:00

Papa Francisko ni Baba wa wote!


Lilian Ndirila Mugombozi ni kati ya vijana ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha watu kushiriki kumpokea na kuadhimisha Mafumbo mbali mbali ya Kanisa na Baba Mtakatifu Francisko wakati huu anapoendelea na hija yake ya kitume nchini Kenya. Anasema Papa Francisko ni Baba wa maskini, mjumbe wa haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Ni kiongozi anayetaka kuona watu wakishikamana na kusaidiana kama ndugu, kumbe ni mjumbe wa umoja na mshikamano kati ya watu. Kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika fikira za ambao baadhi yao walidhani kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anawatembelea waamini wa Kanisa Katoliki peke yao, lakini vijana wamekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wananchi wa Kenya kutambua kwamba, Baba Mtakatifu ni kiongozi wa wote na wala si kwa Wakristo peke yake kwani anataka kukoleza tunu msingi za maisha ya kijamii zinazosimikwa katika utu, heshima, mafao na maendeleo ya wote.

Ni mtu wa watu kwa ajili ya watu! Vijana kwa namna ya pekee wameguswa na ujio wake kwani anataka kuwahamasisha ili kweli waweze kuwa ni vyombo vya Uinjilishaji, haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Baba Mtakatifu Francisko ni chombo muhimu sana cha majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Ujio wa Baba Mtakatifu Francisko utaendelea kuacha chapa ya kudumu katika mioyo ya wananchi wengi wa Kenya wanaokabiliana na changamoto mbali mbali za maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.