2015-11-25 14:41:00

Kenya wekezeni kwa vijana, tunzeni mazingira na pambaneni na vitendo vya kigaidi


Baba Mtakatifu Francisko amewasili nchini Kenya tayari kuanza safari yake ya kitume kwa mara ya kwanza Barani Afrika. Kwenye Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi, Baba Mtakatifu amelakiwa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya aliyekuwa ameandamana na baadhi ya viongozi wa Kanisa na Serikali. Baba Mtakatifu pamoja na ujumbe wake, walielekea Ikulu ya Kenya na huko akapokelewa kwa heshima zote za kitaifa kwa kupigiwa mizinga ishirini na moja pamoja na kutambulishwa baadhi ya wajumbe waliokuwa kwenye msafara wa Rais na ule wa Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao Kenya. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia mambo makuu matatu: umuhimu wa vijana, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kunyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu anatambua umuhimu wa vijana nchini Kenya wanaounda walau asilimia 70% ya idadi ya wananchi wote wa Kenya; kundi muhimu sana katika kukuza na kudumisha demokrasia, heshima, majadiliano, haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, vijana ni rasilimali muhimu sana inapopaswa kulindwa, kukuzwa na kuendelezwa, kwa kujikita katika hekima na tunu msingi za maisha ya kiroho zinazoheshimiwa na kuthaminiwa na wahenga; tunu ambazo zimekita mizizi yake katika mioyo ya watu. Kenya ni nchi ambayo imebahatika kuwa na rasilimali nyingi pamoja na maliasili na kwamba, wananchi wa Kenya wanafahamika sana kwa kuwa na utamaduni wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote.

Uharibifu wa mazingira ni hatari kubwa sana katika ujenzi wa mahusiano kati ya binadamu na mazingira, mwaliko wa kulinda na kutunza mazingira, changamoto kwa wananchi wote lakini kwa namna ya pekee kwa viongozi wa kisiasa kuwa na sera makini zinazolinda na kutunza mazingira kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Lengo anasema Baba Mtakatifu ni kujenga jamii inayosimikwa katika haki na usawa wa kijamii, tayari kusaidia mchakato wa kupyaisha ubinadamu. Jamii ya binadamu inakabiliwa na changamoto kubwa ya kinzani na migawanyiko kwa misingi ya: kikabila, kidini au kiuchumi.

Watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa upatanisho na amani; msamaha na uponyaji wa kweli, ili kujenga jamii inayojikita katika mshikamano, maendeleo, maridhiano, utulivu, daima wakitafuta mafao ya wengi. Uzoefu unaonesha kwamba,  vita, kinzani na vitendo vya kigaidi ni mambo ambayo yanajengeka katika hofu na wasi wasi; hali ya kutoaminiana, hali ya kukata tamaa kutokana na umaskini na watu kuchanganyikiwa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema hawa ni maadui wa amani wanaopaswa kushughulikiwa kikamilifu na watu wote wenye mapenzi mema bila woga wala makunyanzi, kwa njia ya ushuhuda unaojikita katika ukweli, tunu msingi za maisha ya kisiasa na kiroho; tunu ambazo zimekuwa ni mbegu ya kuzaliwa kwa taifa. Tunu hizi kwa namna ya pekee zimedhaminishwa kwa viongozi wa kisiasa, kitamaduni na kiuchumi, dhamana inayohitaji uwajibikaji wa pekee kwa ajili ya huduma kwa wananchi wote wa Kenya, kwani viongozi wamepewa mengi na kwa jinsi hii watadaiwa mengi pia. Watekeleze dhamana hii kwa kuzingatia misingi ukamilifu, uwazi na kwa ajili ya mafao ya wengi, ili kujenga na kuimarisha mshikamano katika ngazi mbali mbali

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anawahamasisha viongozi kuguswa na mahitaji ya maskini; matumaini ya vijana pamoja na mgawanyo bora zaidi wa maliasili na rasilimali watu; mambo ambayo Kenya imebarikiwa kuwa nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kanisa Katoliki litaendelea kuchangia kwa umakini zaidi huduma kwa wananchi wote wa Kenya katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu. Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kuwapongeza wananchi wa Kenya kwa kuwa na utamaduni wa kupanda miti, kielelezo cha maendeleo ya nchi. Anawahimiza kujikita katika mshikamano wa kijamii, haki na amani kwa Kenya na Afrika katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.