2015-11-25 10:43:00

Afrika ni Bara la matumaini yanayokwamishwa na vita, umaskini na migogoro!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 25 Novemba 2015 ameanza hija yake ya kitume Barani Afrika kwa kutembelea: Kenya, Uganda na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Kwenye Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Fiumicino, Baba Mtakatifu amesindikizwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa na Serikali ya Italia. Akiwa njiani kuelekea Barani Afrika kupitia: Italia, Ugiriki, Sudan, Ethiopia na hatimaye Kenya amewatumia salam za matashi mema wakuu wa nchi hizi.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia anasema anatembelea Barani Afrika ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani na anawaombea wananchi wote wa italia mema na ufanisi katika maisha yao. Kwa upande wake, Rais Sergio Mattarella anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa ujumbe wake anapofanya hija ya kitume Barani Afrika. Anasema, Jumuiya ya Kimataifa inaliangalia Bara la Afrika kwa matumaini makubwa kwa ukuaji katika medani mbali mbali za maisha, ingawa hadi sasa vita, migogoro ya kisiasa, umaskini na ukosefu wa usawa kijamii vimekuwa ni vikwazo vikubwa kwa maendeleo ya Bara la Afrika.

Ni matumaini ya Rais Mattarella kwamba, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika utasaidia kuimarisha Jumuiya za Kikristo pamoja na kukoleza mchakato wa amani, udugu na majadiliano katika nchi ambazo zinatembelewa na Baba Mtakatifu na Afrika katika ujumla wake sanjari na kutoa ujumbe wa matumaini kwa Bara la Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.