2015-11-24 10:04:00

Jubilei ya huruma ya Mungu ni dawa katika misigano ya kijamii!


Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma ndiyo mada inayoongoza mafungo ya maisha ya kiroho kwa Wakleri wa Jimbo kuu la Roma, waliojifungia ndani kuanzia tarehe 23 Novemba 2015 kwa ajili ya kusali na kutafakari, tayari kuanza kipindi cha Majilio sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu wakiwa wamejiandaa barabara kukumbatia na kuenzi upendo na huruma ya Mungu, ili waweze kuwa kweli ni vyombo na wagawaji wa huruma ya Mungu kwa watu wanaowahudumia, Jimbo kuu la Roma.

Mafungo haya yatakayohitimishwa hapo tarehe 27 Novemba 2015 yanaongozwa na Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis anaye mshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuitisha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya  huruma ya Mungu, ili kuwasaidia waamini kuambata upendo na huruma ya Mungu inayojikita katika majadiliano, umoja na mshikamano kati ya watu, tayari kuondokana na wasi wasi na woga ambao unaendelea kupandikizwa akilini na mioyoni mwa watu kutokana na vitendo vya kigaidi.

Kardinali Tagle anakaza kusema, Mwaka wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu ni jibu muafaka katika mchakato wa kukabiliana na hofu na wasi wasi katika maisha ya watu kutokana na sababu mbali mbali. Hii ni fursa kwa Mama Kanisa kufanya upembuzi yakinifu katika maisha yake ya kiroho; shughuli za kichungaji na kimissionari ili kukuza na kudumisha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Kanisa kweli liwe ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia waa maisha ya watu.

Mashambulizi na mauaji ya kinyama ni kielelezo cha ukavu wa maisha ya mwanadamu ambao unapaswa kulainishwa kwa njia ya huruma ya Mungu. Watu wanaojihusisha na vitendo vya kigaidi wanakosa ndani mwao chembe ya huruma na mapendo kwa Injili ya uhai. Jubilei ya huruma ya Mungu ni jibu muafaka wa kusitisha vita, mauaji na nyanyaso za kila aina, tayari kuambata huruma na upendo wa Mungu, kwa kutambua kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuuangalia uso wa huruma, “Misericordiae vultus” ili kuonja dhana ya huruma ya Mungu inayojidhihirisha katika dini mbali mbali dunia. Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, iwe ni fursa ya kuambata huruma ya Mungu ambayo ni amana inayovuka mipaka ya Kanisa, kwani ni kielelezo cha sifa njema ya Mwenyezi Mungu ambaye ni Mpole na mwingi wa huruma.

Waamini katika udhaifu na mapungufu yao wasindikizwe na huruma ya Mungu ili kufungua mipaka ya ushirikiano na watu wote wenye mapenzi mema. Mwaka huu iwe ni nafasi ya waamini kufahamiana, kuthaminiana na kuheshimiana kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Uso wa huruma. Ufutilie mbali kiburi cha binadamu, udhalilishaji, ukatili na ubaguzi unaofanywa wakati mwingine kwa misingi ya udini. Kumbe, Jubilei ya huruma ya Mungu iguse maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.