2015-11-24 16:22:00

Baba Mtakatifu Francisko Karibu sana Barani Afrika!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM linapenda kuchukua nafasi hii kumkaribisha kwa moyo mkunjufu Baba Mtakatifu Francisko anapotembelea kwa mara ya kwanza Barani Afrika. Hija hii inafanyika siku chache tu baada ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, fursa makini kwa Baba Mtakatifu kuimarisha Familia ya Mungu Barani Afrika katika imani, matumaini na mapendo. Hii ni nafasi ya kuhimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuweza kujikita katika tunu bora za maisha ya kiafrika na kamba, familia itaendelea kupewa kipaumbele cha pekee kama msingi madhubuti wa jamii. SECAM inawaalika viongozi wa Serikali Barani Afrika kuhakikisha kwamba, wanasaidia kuenzi na kudumisha tunu bora za maisha ya ndoa na familia mintarafu mila na desturi njema za Kiafrika.

SECAM inaungana na viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa kulaani vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia. Wanawataka wale wote wanaowafadhili magaidi kuacha mara moja, ili amani, usalama na utulivu viweze kutawala miongoni mwa jamii. SECAM inapenda kuungana na wapenda amani wote ndani na nje ya Bara la Afrika kuendeleza mchakato wa haki, amani na upatanisho Barani Afrika hususan huko Burundi, Sudan ya Kusini, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, DRC, Nigeria, Kenya, Libya na sehemu mbali mbali za Afrika ya Kaskazini. Huu ni mwaliko wa kuweka silaha chini na kuanza tena mchakato wa majadiliano na amani kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

SECAM inawahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuambata misingi ya haki, amani na upatanisho, wakati huu Familia ya Mungu Barani Afrika inapoadhimisha Mwaka wa Upatanisho, kama sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kichungaji, Dhamana ya Afrika, “Africae munus”. Hii ni changamoto pia ya kukumbatia neema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu,itakayozinduliwa hapo tarehe 8 Desemba 2015. Ni kwa njia hii, Familia ya Mungu inaweza kuambata na kufaidika na huruma pamoja na upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake!

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.