2015-11-23 07:07:00

Yesu Kristo ni Mfalme wa haki, amani na mapendo kwa wote!


Mama Kanisa Jumapili tarehe 22 Novemba 2015 ameadhimisha Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa ulimwengu, ambaye ufalme wake unajikita katika mantiki ya Injili yaani: unyenyekevu, sadaka; katika hali ya ukimya wenye kuwajibisha na katika nguvu ya ukweli. Utawala wake ni tofauti kabisa na watawala wa dunia hii: wenye uchu wa madaraka, wanaoshindana; wanaopigana kwa kutumia silaha za hofu na woga; rushwa na udanganyifu katika dhamiri za watu. Falme za dunia hii wakati mwingine, zinajiimarisha kwa kujitutumua, kinzani na hata dhuluma.

Ufalme wa Kristo una ambata haki, amani na upendo na kwamba; na umejinua kwa namna ya ajabu kabisa katika Fumbo la Msalaba, Yesu aliposhinda dhambi na mauti na kuonesha utukufu wa Msalaba, kielelezo cha sadaka ya Yesu kwa waja wake. Hii ni changamoto kwa Wakristo kufanya rejea katika nguvu ya Fumbo la Msalaba chemchemi ya upendo wa Yesu, hata baada ya kukataliwa na wanadamu, lakini akaonesha ushindi wa kishindo, kwa ajili ya ukombozi wa binadamu.

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme. Alipokuwa ametundikwa Msalabani pale mlimani Kalvari, viongozi wakuu na wapita njia walimdhihaki Yesu wakimtaka ajisalimishe mwenyewe kwa kushuka kutoka Msalabani, lakini Yesu hakutaka kujisalimisha mwenyewe bali alikuja kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kwa kuyamimina maisha yake.

Yule “mwizi mwema” aliyekuwa ametundikwa pembeni mwa Yesu, alimtambua Yesu kuwa ni Mfalme, akamwomba amkaribishe atakapokuwa anaingia kwenye Ufalme wake. Ikumbukwe kwamba, huyu ni mtu ambaye alikuwa amehukumiwa kifo kutokana na matendo maovu aliyoyatenda hapa duniani, lakini akaonja na kushuhudia unyenyekevu na upendo wa Yesu hata alipokuwa pale Msalabani. Baba Mtakatifu anakaza kusema, nguvu ya Ufalme wa Yesu inajikita katika upendo usiokuwa na mipaka; upendo unaomwokoa mwanadamu kutokana katika unyonge na mapungufu yake ya kibinadamu, tayari kumwongoza katika njia ya wema, upatanisho na msamaha.

Mara kwa mara waamini wanapojisikia kuwa ni wanyonge, wanaelemewa na dhambi au hata kushindwa katika maisha yao, wawe na ujasiri wa kumkimbilia Yesu na kumwomba ili aweze kuwaokoa! Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha tafakari yake mbele ya umati mkubwa wa waamini na  mahujaji waliofika mjini Vatican kwa kuwaomba kumkimbilia Bikira Maria ili aweze kuwasaidia kumwiga Yesu Kristo Mfalme katika ulimwengu huu ambao una shida na madonda mengi, ili aweze kuwaonjesha wema, upendo na msamaha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.