2015-11-23 07:49:00

Wajibu wa elimu makini: Kutambua ukweli na wema katika maisha ya mwanadamu!


Kardinali Giuseppe Versaldi, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki wakati alipokuwa anashiriki katika maadhimisho ya Kongamano la Elimu Kimataifa kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Tamko kuhusu Elimu Katoliki “Gravissimum educationis” na miaka 25 ya Tamko kuhusu vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu za Kanisa Katoliki “Ex corde Ecclesiae”, amewataka wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanatoa elimu makini kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Sera ya elimu inayotolewa na Kanisa Katoliki inajikita katika msingi wa Injili, unaopania kuchochea majadiliano ya kina kati ya: Familia, Kanisa, Jamii na Serikali, ili kuweza kupata elimu makini inayoendana na mazingira ya watu wa nyakati hizi. Huu ni mwaliko kama walivyosema Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican  wa kusoma alama za nyakati. Kongamano hili limekuwa likiendeshwa mjini Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma na Jumamosi, tarehe 21 Novemba 2015 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko aliyejibu maswali mbali mbali yaliyoulizwa na wajumbe waliokuwa wanashiriki katika kongamano la Elimu Katoliki Kimataifa.

Kardinali Versaldi amekazia umuhimu wa haki ya watoto kupata elimu makini, kama sehemu ya utekelezaji na udumishaji wa utu na heshima ya binadamu, bila ubaguzi wala upendeleo, jambo ambalo kwa sasa ni changamoto kubwa katika sekta ya elimu sehemu mbali mbali za dunia. Lakini haya ni mambo ambayo Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican waliyapatia kipaumbele cha pekee, ili Kanisa liweze kuchangia katika ustawi na maendeleo ya wengi kwani sekta ya elimu ni sehemu ya utekelezaji wa utume na dhamana ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Inasikitisha kuona kwamba, leo hii kuna watoto zaidi ya millioni 58 ambao hawajapata fursa ya kwenda shule; hawa ni watoto wenye umri kati ya miaka sita hadi kumi na moja; matumaini ya watoto hawa kwa siku za usoni yako hatarini. Shule, taasisi za elimu na vyuo vikuu vinapaswa kuwa ni mahali pa salama, ili kutoa nafasi kwa wanafunzi kujifunza kwa umakini mkubwa, lakini zimekuwa pia ni sehemu ya mashambulizi ya kigaidi pamoja na vita vinavyoendelea kufuka moshi sehemu mbali mbali za dunia. Kuna baadhi ya wanafunzi wanabaguliwa na kutengwa; wana nyanyaswa na kudhalilishwa anasema Kardinali Versaldi. Baadhi ya serikali zinaendelea kuzibagua taasisi zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki.

Kuna baadhi ya nchi kama vile: Burundi, Rwanda, Ghana, Yemen, Nepal, India, Iran na Vietnam ambazo zimefanikiwa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya watoto ambao hawakuwa wamepata fursa ya kwenda shule, ingawa bado kuna safari kubwa ya kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na maboresho makubwa ya kiwango na ubora wa elimu inayotolewa. Wanafunzi wanapaswa kujengewa uwezo ili kweli wawe ni mashuhuda wa ukweli na wema; mambo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya mtu. Elimu Katoliki inalenga kwa namna ya pekee kabisa kuunganisha weledi na utu wa mtu.

Professa Italo Fiorin kutoka Chuo kikuu cha LUMSA kilichoko hapa mjini Roma amegusia matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika sekta ya elimu: kwanza kabisa na utambulisho wa Elimu Katoliki; umuhimu wa kuwa na elimu inayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; Majiundo na malezi kwa watoto wanaotoka katika pembezoni mwa jamii na katika familia maskini; mwendelezo wa mchakato wa Elimu Katoliki.

Askofu mkuu Angelo Zani, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki amepitia kwa muhtasari mafanikio, matatizo na changamoto ambazo zimejitokeza katika kipindi cha miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Tamko kuhusu Elimu Katoliki na Miaka 25 ya Tamko kuhusu Taasisi za elimu ya juu na Vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki. Amewapongeza wajumbe kwa kushirikisha kwa kina na mapana mawazo ambayo yatafanyiwa kazi ili kuwa na mwelekeo mpya katika sekta ya elimu inayotolewa na Kanisa Katoliki sanjari na kuendelea kusoma alama za nyakati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.