2015-11-23 09:30:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Familia ya Mungu Kenya na Uganda


Baba Mtakatifu Francisko wakati huu anapojiandaa kwa ajili ya kuanza hija yake ya kitume Barani Afrika kwa kutembelea: Kenya, Uganda na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, ametuma ujumbe wa matashi mema na urafiki kwa Familia ya Mungu Barani Afrika; ana matumaini makubwa kwamba, watapata nafasi ya kukutana na kuzungumza kwa pamoja. Anakaza kusema, anakuja Barani Afrika kama mjumbe wa Injili, ili kuwatangazia watu upendo wa Yesu unaojikita katika upatanisho, msamaha na amani.

Lengo la hija hii ya kitume anasema Baba Mtakatifu ni kutaka kuwaimarisha ndugu zake katika imani, ili waweze kuwa mashuhuda wa Injili inayofundisha na kutetea utu na heshima ya binadamu; tayari kufungua mioyo kwa wengine, hususan maskini na wahitaji zaidi. Anakaza kusema, anatamani kukutana na Familia ya Mungu nchini Kenya na Uganda katika ujumla wake, ili kuwapatia neno la faraja, hususan wakati huu ambapo kuna changamoto nyingi za kidini. Kumbe, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kufahamiana, kuheshimiana na kushikamana kama ndugu wamoja katika familia ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema  kwamba, binadamu wote ni watoto wa Mwenyezi Mungu. Kwa namna ya pekee, anapenda kukutana na kuzungumza na vijana, rasilimali muhimu sana na chachu ya matumaini kwa kesho inayojikita katika mshikamano, amani na ustawi. Baba Mtakatifu anapenda kutumia nafasi hii kuwashukuru wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza ili kufanikisha hija yake ya kitume Barani Afrika. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza kwa sala ili hija yake ya kitume nchini Kenya na Uganda iwe ni chemchemi ya matumaini na ari mpya kwa wote. Mwishoni, anawapatia baraka zake za kitume, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia furaha na amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.