2015-11-23 08:43:00

Papa Francisko anataka kuimarisha mchakato wa haki, amani na upatanisho Afrika


Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anasema, Baba Mtakatifu Francisko anatembelea Barani Afrika kama mjumbe wa haki, amani na upatanisho kati ya watu. Ratiba yake itaendelea kuheshimiwa kadiri ya mazingira yanavyoruhusu na kwamba, kwa sasa hakuna mabadiliko yoyote, hata kama hali ya ulinzi na usalama ni tete Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Vatican inaendelea kufuatilia matukio yote haya kwa karibu zaidi na kwamba, Baba Mtakatifu hana wasi wasi kuhusu maisha yake.

Bwana Domenico Giani, Kamanda mkuu wa vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican yuko tayari Barani Afrikaili kuweza kujiridhisha na maandalizi kwa ajili ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika. Akiwa Barani Afrika, Baba Mtakatifu anatarajiwa kutumia gari la wazi, ili kuonana na kukutana na umati mkubwa wa familia ya Mungu, jambo ambalo Baba Mtakatifu anapenda kulipatia kipaumbele cha pekee.

Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Kenya, Uganda na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati anatarajiwa kutoa hotuba na mahubiri 19, yatakayokuwa kwa lugha ya Kiitalia, hotuba 2 kwa lugha ya Kiingereza, hotuba 2 kwa lugha ya Kihispania na hotuba 1 kwa lugha ya Kifaransa. Padre Lombardi anasema, kwa mara ya kwanza Baba Mtakatifu Francisko atazungumza kwa lugha ya Kifaransa hadharani, jitihada za kutaka kufikisha ujumbe wake moja kwa moja katika mioyo ya watu!

Baba Mtakatifu akiwa nchini Kenya atapenda kukazia umuhimu wa majadiliano ya kidini kama sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha haki, amani na maridhiano, ili watu waweze kujikita katika utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Atahimiza utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, atakapotembelea ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Nairobi.

Padre Lombardi anakaza kusema, kutokana na umuhimu wa tema hii ya mazingira, Kardinali Pietro Parolin, katibu mkuu wa Vatican itambidi kuondoka mapema Barani Afrika, ili kuelekea mjini Paris, Ufaransa kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi; mambo ambayo yanaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika balaa la njaa na umaskini mkubwa!

Papa Francisko ni Baba wa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, atapenda kukutana na kuzungumza na watu wanaoishi katika mazingira duni kwenye kitongoji cha Kangemi, nje kidogo ya Jiji la Nairobi, ili wao pia watambue kwamba, Kanisa linawaheshimu na kuwathamini kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; utu wao unapaswa kudumishwa na wote.

Baba Mtakatifu akiwa nchini Uganda atatoa heshima yake ya pekee kwa mashuhuda wa imani walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; damu yao ikawa ni mbegu ya Ukristo ndani na nje ya Uganda. Ushuhuda wa imani tendaji ni kati ya mada ambazo Baba Mtakatifu Francisko anazipatia umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa.

Jumapili tarehe 29 Novemba 2015, Baba Mtakatifu akiwa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kufungua lango la maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, tayari kuwaonesha waamini kwamba, Kristo ndiye mlango wa uzima wa milele. Kumbe, waamini wanahamasishwa kwa namna ya pekee, kuambata upendo na huruma ya Mungu, tayari kufanya toba na wongofu wa ndani, ili kweli waweze kuwa ni vyombo vya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Akiwa Bangui, Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kutembelea kambi ya wakimbizi na wahamiaji, ili kuwafariki na kuwapatia matumaini mapya katika  maisha, licha ya hali ngumu wanayokabiliana nayo kwa sasa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.