2015-11-23 07:18:00

Nisindikizeni kwa sala na sadaka zenu, ili Afrika iweze kuwa na amani na ustawi!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ameyaelekeza mawazo yake Barani Afrika kwa kuwaambia waamini kwamba, Jumatano ijayo tarehe 25 Novemba 2015 anatarajia kuanza hija yake ya kitume Barani Afrika kwa kutembelea: Kenya, Uganda na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.

Baba Mtakatifu anawaomba na kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza katika hija hii kwa njia ya sala na sadaka zao, ili hija hii iwe kweli ni kielelezo cha uwepo wake wa karibu na upendo kwa Familia ya Mungu Barani Afrika. Anawaomba kumwomba Bikira Maria kweli aweze kusaidia nchi hizi kujikita katika amani na maendeleo ya kweli.

Baba Mtakatifu amewakumbuka, Mwenyeheri Federico Berga na wenzake ishirini na watano waliotangazwa na Mama Kanisa kuwa Wenyeheri, Jumamosi iliyopita tarehe 21 Novemba 2015, huko Barcellona, Hispania. Wenyeheri hawa waliuwawa kikatili wakati wa madhulumu ya Kanisa, kwenye Karne iliyopita. Hawa ni Mapadre, watawa waliokuwa wanajiandaa kwa ajili ya kupewa Daraja Takatifu pamoja na walei waliowekwa wakfu katika Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Francisko, yaani Wakapuchini. Baba Mtakatifu amewaweka chini ya ulinzi na tunza yao, waamini wote wanaoendelea kuteswa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.