2015-11-23 15:43:00

Miaka 54 ya Uhuru wa Tanzania hakuna mnuso wa kitaifa!


Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli ameagiza siku ya sikukuu ya Uhuru, 9 Desemba hakutakua na sherehe za kitaifa na badala yake watu watatumia siku hiyo kufanya usafi katika maeneo yao. Maamuzi haya yamekuja siku chache baada ya Dk.Magufuli kutoa tena agizo la fedha zaidi ya milioni 250 ambazo zilikuwa zitumike kwenye sherehe za ufunguzi wa Bunge, Dodoma kuelekezwa kwenye ununuzi wa vitanda vya wagonjwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili. 

Rais amechukua maamuzi hayo kutokana na kukerwa na ugonjwa wa kipindupindu ambao tayari umepoteza maisha ya watu na bado umeendea kukumba maeneo mbalimbali nchini Tanzania. Kwa niaba ya Rais, Katibu Mkuu kiongozi Ombeni Sefue baada ya kufanya ziara katika Hospitali ya taifaMuhimbili alisema Rais ameagiza kuwa siku hiyo hakutakuwa na sherehe zozote za kitaifa na badala yake wananchi wataitumia kufanya usafi katika maeneo yao.

“Rais amesema suala la kuwepo ugonjwa Kipindupindu halikubaliki, jambo hili limemkera sana, tunasherehekea miaka 54 ya uhuru lakini bado kipindupindu kinatusumbua sana, amesema kama Watanzania lazima tulishughulikie, haiwezekani akija mgeni kama Obama tunafanya usafi lakini akiondoka tunaendelea kuwa wachafu, ameamua tarehe 9 Desemba siku ya uhuru hakutakuwa na sherehe yoyote badala yake watu wakasafishe maeneo yao”..Ombeni Sefue.

Ombeni Sefue aliongeza kuwa “Amesema hakutakuwa na cha kwenda kwenye Gwaride, kila mkuu wa Mkoa au kiongozi yeyote wa eneo husika wanatakiwa waanze kuandaa vifaa vya usafi, itakuwa ni siku ya kufanya usafi ili kupunguza tatizo la uchafu..ameowaomba sana Watanzania si kwamba tuna dharau siku hii bali tunaifanya kwa staili nyingine…kuhusu gharama za sherehe pesa zitakazotumika siku hiyo Rais atatafuta kazi ya kuzifanyia, atazipeleka kwenye eneo lingine lenye tatizo “..Ombeni Sefue. Sefue aliongeza kuwa Rais amesema hatapenda kusikia baada ya Desemba kuna maeneo bado yatakuwa na ugonjwa wa Kipindupindi na Mkoa ambao utakuwa bado na ugonjwa huo viongozi wake watajieleza.

Na Mwandishi maalum

 








All the contents on this site are copyrighted ©.