2015-11-23 11:47:00

Gavana mkuu Williams akutana na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 23 Novemba 2015 amekutana na kuzungumza na Bwana Rodney Williams, Gavana mkuu wa Antigua na Barbuda, ambaye baadaye amekutana pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo kati ya viongozi hawa wawili, wamepongeza uhusiano mwema uliopo kati ya pande hizi mbili, hali ambayo imeimarishwa kwa kuwa na balozi anayeiwakilishi nchi hii mjini Vatican. Wamegusia pia mchako wa Kanisa katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Antigua na Barbuda katika mchakato wa kulinda, kutetea na kudumisha utu wa binadamu sanjari na huduma makini katika sekta ya elimu na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni matumaini ya viongozi hawa wawili kwamba, mahusiano haya yataendelezwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya pande hizi mbili. Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake wamejadili pia masuala muhimu ya kikanda na kimataifa hususan kuhusiana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sanjari na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.