2015-11-23 07:32:00

Baba Mtakatifu Francisko arejea darasani kupembua changamoto za elimu!


Kongamano la Elimu Kimataifa lililoandaliwa na Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipotoa Tamko kuhusu Elimu Katoliki “Gravissimum educationis” Miaka 25 ya Tamko kuhusu vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, “Ex corde Ecclesiae” kwa kuwashirikisha wadau kutoka sehemu mbali mbali za dunia, limehitimishwa, Jumamosi iliyopita tarehe 21 Novemba 2015 kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.

Wajumbe walitumia nafasi hii kumuuliza maswali Baba Mtakatifu Francisko naye akawajibu kwa kina na mapana kwa kukazia: umuhimu wa Serikali kuhakikisha kwamba waalimu wanalipwa mishahara mizuri ili waweze kutekeleza dhamana na wito wa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ujuzi na maarifa, tayari kupambana na mazingira, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Waalimu wanafanya kazi kubwa sana ya kumwendeleza mwanadamu na kwamba, elimu bora inapaswa kutolewa kwa wote pasi na ubaguzi kati ya maskini na matajiri. Baba Mtakatifu alibahatika kusikiliza shuhuda zilizotolewa na wadau mbali mbali kutoka Afrika, Nchi Takatifu, India, Rione na Italia, wadau ambao wako mstari wa mbele katika sekta ya elimu inayotolewa na Mama Kanisa hususani miongoni mwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu Francisko akijibu swali la kwanza kuhusu ufundishaji wa Elimu Katoliki katika mazingira ya watu wenye dini na imani mbali mbali duniani, alikazia umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; Elimu Katoliki isaidie kukuza majadiliano ya kitamaduni, kidini na kiekumene kwa njia ya taasisi zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia.

Lengo ni kuwawezesha watu kutambua Fumbo la Umwilisho, ambalo kwalo Neno wa Mungu amefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake. Elimu Katoliki haimaanishi kuwafundisha wanafunzi Katekesi peke yake, bali kuhakikisha kwamba, tunu msingi za maisha ya Kikristo zinamwilishwa miongoni mwa wanafunzi, ili waweze kuwa kweli ni mashuhuda wa haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu. Wanafunzi waelimishwe tunu bora za maisha ya kiutu na kimaadili, tayari kuwa kweli ni raia wema na watu wanaowajibika katika maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, leo hii wanafunzi wanafundishwa mambo ya kidunia na kusahau mambo ya maisha ya kiroho, hali inayopelekea wanafunzi wengi kukengeuka. Kumbe, kuna haja kwa taasisi za elimu zinazoendeshwa na Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia kuwa wazi ili kuwasaidia watu kutambua mambo msingi ya maisha ya kiroho na kiutu, kwa kuwa na mwelekeo mpana zaidi na kamwe Kanisa lisijitafute lenyewe bali liwe ni sehemu ya mchakato wa huduma kwa binadamu kwani kujifungia lenyewe hakusaidii na wala hakuna mashiko!

Baba Mtakatifu ameonesha uhusiano mkubwa uliopo kati ya familia na shule na kuonesha masikitiko yake kwamba, elimu kwa watu wa nyakati hizi imekuwa na mwelekeo wa ubaguzi kwa kutoa elimu bora zaidi kwa matajiri na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”, kuambulia makombo ya elimu elimu duni. Elimu inapaswa kusaidia mafungamano ya kijamii kwa kujenga umoja na mshikamano na kwamba, kuna haja kwa jamii kuhakikisha kwamba, zinajenga na kuimarisha ushirikiano kati ya familia na shule, ili kuweza kupata matokeo makubwa zaidi.

Baba Mtakatifu anaendelea kukazia kwamba, ushirikiano kati ya familia, shule na serikali ni muhimu sana, ili kuhakikisha kwamba, walimu wanalipwa vizuri ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao nyeti ndani ya jamii. Walimu wasipolipwa vyema “watayakoroga” na matokeo yake ni kuyumba kwa msingi wa elimu katika jamii. Mtakatifu Yohane Bosco, alikazia umuhimu wa familia, shule na serikali kushirikiana, ili kupata mafanikio makubwa zaidi.

Baba Mtakatifu Francisko anasema utoaji wa elimu makini hauna budi kuwashirikisha watu wote na wala asiwepo mtu hata mmoja anayetengwa wala kubaguliwa. Elimu ijitahidi kuingia katika vichwa, mioyo na mikono ya watu, huu ndio mwelekeo mpya ambao elimu inapaswa kuelekezwa. Lengo ni kuwafundisha wanafunzi kufikiri vyema; kuwasaidia kujisikia vyema na kuwasindikiza ili waweze kutenda mambo mema katika maisha yao.

Kwa njia hii elimu inatoa nafasi kwa kila mwanafunzi kushiriki kikamilifu na wala hakuna nayebaguliwa wala kutengwa. Mwelekeo wa sasa ni kutoa elimu bora kwa watoto wanaotoka kwenye familia zenye uwezo mkubwa zaidi na maskini wanaendelea kubaki wakiwa wameng’ang’ania mkiani. Lakini ikumbukwe kwamba, elimu ni mkombozi wa wote.

Dunia haitaweza kupata mafanikio katika sekta ya elimu ikiwa kama itajikita katika sera za kibaguzi, kumbe, changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, mchakato wa elimu unawasaidia wanafunzi kupambana na mazingira yao kwa kuwapatia: ujuzi na maarifa; kanuni maadili na utu wema bila kusahau kuwafundisha mambo msingi katika maisha ya kiroho, ili kumuunda mtu mzima: kiroho na kimwili. Mfumo wa elimu baguzi anakaza kusema Baba Mtakatifu unatafuta faida kubwa kwa watu wachache na maangamizi kwa binadamu wengi. Wazazi wanapaswa kuwekeza zaidi katika elimu bora kwa watoto wao.

Baba Mtakatifu anawataka wadau mbali mbali wa elimu kuhakikisha kwamba, wanakwenda pembezoni mwa jamii ili kuwasaidia vijana kupata elimu makini itakayowawezesha kuwa kweli ni vyombo vya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Jamii isipofanya hivyo, vijana watajikuta wanatumbukizwa kwenye mikono ya walimu wengi watakaosababisha uvunjifu wa amani, maadili na utu wema. Vijana walioko pembezoni mwa jamii wafundwe kutambua na kuheshimu utu wa binadamu na haki zake msingi; wakuze ufahamu, ujuzi na maarifa; kwa kujikita katika tunu bora za maisha ya kiroho na kiutu, ili mwisho wa siku waweze kuwashirikisha wengine uzuri wa kukanyaga umande!

Umefika wakati wa kuvunjilia mbali kuta zinazowatengenisha watu katika sekta ya elimu kwa kutoa upendeleo kwa wenye fedha na kuwasahau maskini. Mtakatifu Yohane Bosco awe kweli ni mfano wa kuigwa katika mchakato wa kuwapatia vijana wa kizazi kipya elimu bora na makini katika maisha yao, tayari kupambana na mazingira, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri pa kuishi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.