2015-11-21 07:43:00

Papa Francisko kukazia: Majadiliano, Mazingira, Ushuhuda na Jubilei ya huruma


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Kituo cha televisheni cha Vatican anasema, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika kuanzia tarehe 25- 30 Novemba 2015 atapenda kukazia umuhimu wa mchakato wa majadiliano ya kidini; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu pamoja na ushuhuda wenye mvuto na mashiko kutoka kwa  Familia ya Mungu Barani Afrika, wakati huu Kanisa Barani Afrika linapoendelea kuadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Kanisa lilipowatangaza Mashahidi wa Uganda.

Kardinali Parolin anasema, Baba Mtakatifu Francisko anatembelea Barani Afrika kama mjumbe wa haki, amani na maridhiano kati ya watu. Anapenda kuwaimaarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo, ili waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa mchakato wa upatanisho unaojikita katika majadiliano ya kidini, kwa kufumbata: ukweli na uwazi kwa ajili ya mafao ya wengi. Misimamo mikali ya kidini imekuwa ni chanzo kikuu cha maafa ya watu na mali zao kama ilivyotokea hivi karibuni huko Paris, Ufaransa zaidi ya watu 133 kupoteza maisha; kama ilivyokuwa Garissa nchini Kenya, wanafunzi 147 walipouwawa kikatili.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukemea vitendo vya kigaidi vinavyofanywa kwa kisingizio cha udini, jambo ambalo ni kashfa kubwa kwa Mwenyezi Mungu ambaye kimsingi ni chemchemi ya upendo, unaopaswa kumwilishwa kwa jirani. Dini zinapaswa kuwa kweli ni vyombo vya amani, wema, haki, upatanisho na udugu duniani. Hii ni changamoto kwa dini mbali mbali kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu: kiroho na kimwili.

Ni mwaliko wa dini mbali mbali duniani kuwa chachu ya udugu na mshikamano; mambo yanayoweza kutekelezwa kwa njia ya majadiliano ya kidini. Haya ni mambo msingi ambayo Baba Mtakatifu Francisko angependa kuyapatia kipaumbele cha pekee wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika.

Kardinali Parolin anakaza kusema, utunzaji bora wa mazingira, sera na uchumi unaojali mahitaji msingi ya binadamu dhidi ya umaskini na ubaguzi ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko anayakazia kama sehemu ya utekelezaji wa Mafundisho Jamii ya Kanisa, changamoto iliyotolewa kuanzia kwa Papa Leo wa XIII. Kanisa linapenda kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: maisha, utu na heshima ya binadamu. Rasimali ya dunia inapaswa kutumiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi na kwamba, utu na heshima ya watoto wa Mungu Barani Afrika haina budi kuheshimiwa na kuthaminiwa. Mapambano dhidi ya umaskini ni changamoto pevu Barani Afrika anasema Kardinali Parolin.

Baba Mtakatifu akiwa nchini Kenya atapata fursa ya kutembelea Makao makuu ya Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayojihusisha na mazingira pamoja na makazi ya watu. Itakumbukwa kwamba, mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi utafanyika wakati Baba Mtakatifu Francisko akiwa Barani Afrika. Jijini Nairobi, kutafanyika pia mkutano wa mawaziri wa biashara mara tu baada ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Kenya. Zote hizi ni juhudi za Jumuiya ya Kimataifa kutaka kuibua mbinu mkakati unaojikita katika kanuni maadili, ili kweli sera za uchumi ziwe ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Kiini cha hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Barani Afrika ni Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, ambako anatarajiwa kufungua lango la maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. Itakumbukwa kwamba, uzinduzi rasmi wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu ni hapo tarehe 8 Desemba 2015. Baba Mtakatifu anapenda kuwaonesha watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati upendo na mshikamano wake kutokana na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo, ikiwemo vita, magonjwa na ukosefu wa fursa za ajira.

Kardinali Parolin anakaza kusema, itakuwa ni fursa ya kuwahimiza wananchi kuanza mchakato wa majadiliano ya kidini na kitamaduni katika ukweli na uwazi, ili kuganga na kuponya madonda ya chuki na uhasama ambayo yamejitokeza miongoni mwao katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Ni muda wa kuandika ukurasa mpya wa umoja na mshikamano wa kitaifa, kwa ajili ya ustawi na maendeleoya wengi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu na wala si kama adui. Baba Mtakatifu atapenda kuwahamasisha watu wote wenye mapenzi mema wanaotaka kuchangia katika mchakato wa ustawi na maendeleo ya Afrika ya Kati, kujitokeza bila kusita, licha ya magumu na changamoto wanazoweza kukabiliana nazo!

Kardinali Parolin anafafanua kwamba, Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Uganda atashiriki katika mwendelezo wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mashahidi wa Uganda walipotangazwa kuwa Watakatifu. Hawa ni mashuhuda wa imani tendaji inayopaswa kushuhudiwa na Familia ya Mungu Barani Afrika kama alivyokaza kusema Mwenyeheri Paulo VI wakati alipokuwa anawatangaza Mashahidi wa Uganda kuwa Watakatifu. Yesu Kristo mkombozi wa dunia anapaswa kuwa ni kiini na rejea ya maisha ya Wakristo wote. Damu ya mashuhuda wa imani ni mbegu ya Ukristo sehemu mbali mbali za dunia na chachu ya ujenzi wa umoja na udugu; haki na amani; upendo na mshikamano kwa ajili ya mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.