2015-11-21 08:59:00

Mwaka wa Wanaume Wakatoliki Jimbo kuu la Mwanza moto wa kuotea mbali!


Maadhimisho ya Mwaka wa Wanaume Wakatoliki Jimbo Kuu la Mwanza ni tukio la kihistoria katika Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Jimbo Kuu la Mwanza, mwanzo mpya katika maisha na utume wa Kanisa Jimbo kuu la Mwanza. Familia ya Mungu Jimboni humu inaendelea kuwekeza katika mafanikio yaliyopatikana wakati wa maadhimisho ya Mwaka wa imani pamoja na Mwaka wa Familia, lengo ni kuwawezesha waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku hasa Mwaka huu Kanisa linapoadhimisha pia Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Mwaka wa Wanaume Wakatoliki Jimbo kuu la Mwanza ni”Mwanaume mkatoliki: mhimili imara wa taifa la Mungu”.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Mwanza anasema, maadhimisho ya Mwaka wa Wanaume Wakatoliki Jimbo kuu la Mwanza ulizunduliwa hapo tarehe 22 Machi 2015 na utahitimishwa rasmi mwaka 2016. Mwaka huu unapania kuenzi tunu ya wanaume na ubaba ndani ya: Familia, Kanisa na Jami katika ujumla wake. Ni fursa kwa wanaume Wakatoliki kujitazama na kujitathmini kwa unyofu na ukweli; ili waweze kujikubali, kuwajibika na kung’ara kama vyombo makini katika kazi ya Uumbaji na Ukombozi ndani ya Kanisa na Jamii.

Mwaka unaowapatia wanaume Wakatoliki nafasi ya kutambua na kutafakari juu ya wito na utume wao; kuleta mwamko mpya ndani ya Kanisa; kuboresha ushiriki na ushirikishwaji wa wanaume katika maisha na utume wa Kanisa, pamoja na kuwahimiza wanaume kujituma zaidi. Kuamsha na kujenga ari na mwamko wa Uinjilishaji na Umissionari mpana ili kukabiliana na changamoto katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Ni mwaliko kwa wanaume kujitokeza zaidi ili kujikita katika changamoto ya kuambata utakatifu, tayari kushiriki kikamilifu katika kuyatakatifuza malimwengu, huku wakiendelea kuwa ni nuru ya mataifa na chumvi ya dunia. Biblia na Msalaba ndivyo vielelezo vikuu vya maadhimisho ya Mwaka wa Wanaume Wakatoliki Jimbo kuu la Mwanza, chini ya usimamizi na maombezi ya Mtakatifu Yosefu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.