2015-11-21 14:35:00

Hazina ya ujumbe wa Yohane Paulo II alipotembelea Kenya!


Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya anawahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujitokeza kwa wingi kabisa kumpokea Baba Mtakatifu Francisko wakati atakapowasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Jumatano tarehe 25 Novemba 2015 na baadaye wakati wa maadhimisho ya matukio mbali mbali nchini Kenya.  Kanisa nchini Kenya linaendelea kuwahamasisha watu wote wenye mapenzi mema kujitokeza kumwona na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjumbe wa amani anayewatembelea ili kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu akiwa nchini Kenya atabahatika kukutana na familia ya Mungu katika ujumla wake.

Padre Paschal Mwijage, SJ, Paroko wa Parokia ya Mt. Yosefu Kangemi ni kati ya Maparoko wenye furaha kubwa nchini Kenya kwa kupata bahati ya Baba Mtakatifu Francisko kutembelea katika eneo lake, mahali ambapo kuna makazi yasiyo rasmi na watu wanaishi katika mazingira magumu! Uwepo wa Baba Mtakatifu katika eneo hili ni kutaka kuwaimarisha wananchi kupambana kufa na kupona katika mchakato wa maboresho ya maisha yao, ili kulinda na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu. Ni mwaliko kwa viongozi wa Serikali na kijamii kushughulikia matatizo ya wananchi kwa kutumia vyema rasimali ya nchi kwa mafao ya wengi. Hata katika umaskini wao, Baba Mtakatifu anataka kuwaimarisha katika misingi ya imani, haki na mapendo!

Itakumbukwa kwamba, hii ni mara ya nne Kenya inatembelewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa mara ya kwanza Kenya ilitembelewa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1980; mara ya pili kunako mwaka 1985 ili kushiriki katika maadhimisho ya Kongamano la  43 la Ekaristi Takatifu Kimataifa; mara ya tatu ni pale Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Kenya ili kuzindua Hati ya kichungaji, Kanisa Barani Afrika, Ecclesia in Africa kunako mwaka 1995 na sasa Baba Mtakatifu Francisko anaitembelea Familia ya Mungu nchini Kenya, matendo makuu ya Mungu.

Mtakatifu Yohane Paulo II nyakati zote za hija zake za kichungaji nchini Kenya amekazia kwa  namna ya pekee umoja na mshikamano wa kitaifa miongoni mwa Familia ya Mungu nchini Kenya na kwamba, Kanisa lilikuwa linahimizwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa familia ya binadamu nchini Kenya kwa kuwajibika bararaba. Aliwataka wananchi wa Kenya kuepuka kabisa siasa, sera na mikakati inayopingana na tunu msingi za maisha ya Kiafrika na Kikristo,  kwa kuambata: mafao ya wengi, uhuru wa kuabudu na kusimama kidete kupinga aina zote za ubaguzi mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Papa Yohane Paulo II aliwataka wananchi wa Kenya kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi katika nchi yao sanjari na kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kuimarisha mafungamano ya kijamii, maridhiano na kukuza amani na umoja wa kitaifa. Aliwashauri pia wanadiplomasia kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kujitahidi kuendeleza utambulisho wa Mwafrika kwa kumwangalia mintarafu mwanga wa Kristo Yesu. Alilitaka Kanisa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha sera za utunzaji bora wa mazingira kwa kujikita katika ekolojia ya binadamu kama kikolezo cha haki, amani na maridhiano kati ya watu. 

Papa Yohane Paulo II alikaza kusema, familia ni shule ya kwanza kabisa ya tunu msingi za maisha ya kiroho na kijamii, ni shule ya sala, toba na wongofu wa ndani. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema walihamasishwa kujenga utamaduni wa kusikiliza Neno la Mungu, kurutubisha maisha yao ya kiroho kwa Sakramenti za Kanisa, ili kujenga na kuimarisha Jumuiya inayojikita katika fadhila ya upendo; Injili ya uhai, imani na matumaini. Alikazia kwa namna ya pekee juu ya utume wa familia ili familia za Kikristo ziweze kutekeleza dhamana na wajibu wake kikamilifu. Ili kufanikisha azma hii, kulikuwa na haja ya kuendeleza Katekesi makini miongoni mwa familia.

Mtakatifu Yohane Paulo II aliwataka viongozi wa Kanisa nchini Kenya kukuza dhana ya utamadunisho na kuwa na mikakati makini ya majiundo na malezi ya awali na endelevu kwa Wakleri ili waweze kutekeleza wajibu wao barabara ndani ya Kanisa na Jamii inayowazunguka. Maaskofu na Mapadre waoneshe na kushuhudia moyo wa umoja, upendo na mshikamano kama mihimili mikuu ya Uinjilishaji. Ushuhuda huu ujioneshe kwa namna ya pekee katika utakatifu wa maisha. Wakleri wanakumbushwa kwamba wao ni wahudumu wa Neno, Sakramenti na Maisha ya Kanisa!

Papa Yohane Paulo II aliwakumbusha waamini kwamba, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya maisha; ni shule ya sala, imani na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu na kwamba, hii ni sakramenti muhimu sana katika maisha ya ndoa na familia. Hapa waamini wanajichotea nguvu itakayowasaidia kujikita katika utakatifu wa maisha, tayari kuyatakatifuza malimwengu. Kwa ufupi haya ni kati ya mambo ambayo yamekaziwa na Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alipotembelea nchini Kenya katika safari zake tatu za kichungaji! Kwa sasa Kenya wako moto kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko anapowatembelea!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.