2015-11-21 14:14:00

Familia zinahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya familia!


Askofu James Maria Wainaina Kungu wa Jimbo Katoliki la Murang’a Kenya, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anazungumzia kuhusu umuhimu wa familia katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili pamoja na hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Kenya. Familia ina dhamana yake katika kazi ya ukombozi kama inavyojionesha tangu mwanzo wa kuumbwa kwa ulimwengu, katika maisha ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, katika Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu; mambo ambayo yameendelea kupewa msukumo wa pekee na Mababa wa Kanisa kwa nyakati mbali mbali. Familia ni chimbuko la maisha; ni shule ya utakatifu, haki na amani na mapendo thabiti na utimilifu wa maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji mpya.

Familia ni kielelezo cha mkamilishano katika mafungamano ya maisha ya kijamii, kutokana na dhamana na utume huu, familia zinapaswa kuwa ni vyombo vya Uinjilishaji kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Ushuhuda unaojikita kwa namna ya pekee katika maisha ya kiroho, kanuni maadili na utu wema. Familia kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mambo msingi, zitaweza anasema Askofu James Wainaina kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya familia inayofumbata zawadi ya maisha!

Familia ina utume mahususi sana ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake, kumbe familia inapaswa kufundwa tangu mwanzo wa wanandoa watarajiwa wanapoanza kuchumbiana, wasindikizwe katika maadhimisho ya Sakramenti ya Ndoa Takatifu na kwamba, kuna haja kwa Kanisa kuwa na Wakleri waliofundwa barabara ili kusaidia utekelezaji wa utume wa familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo. Kwa njia hii kweli familia zitaweza kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Uinjilishaji kwa kujikita katika utakatifu wa maisha, chachu muhimu sana katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Akizungumzia kuhusu hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Kenya kuanzia tarehe 25- 27 Novemba 2015 anakaza kusema kwamba, alipata nafasi ya kuzungumza na Baba Mtakatifu wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya familia na kumhakikishia kwamba, yuko tayari kukutana na Familia ya Mungu nchini Kenya. Askofu James Wainaina anasema, amemhakikishia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema wanaendelea kufanya maandalizi: kiroho na kimwili, ili kumpokea na kumkaribisha miongoni mwao. Wako tayari kupokea ujumbe na changamoto kwa Familia ya Mungu Barani Afrika.

Askofu Wainaina anakaza kusema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika ni kutaka kuimarisha imani, matumaini na mapendo miongoni mwa familia ya Mungu, ili wananchi waweze kuwa ni vyombo na wajenzi wa madaraja ya watu kukutana, kusaidiana huku wakiheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja pasi na ubaguzi. Lengo ni kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, mshikamano na maridhiano kati ya wananchi wote wa Kenya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.