2015-11-20 14:52:00

Rais Petro Poroshenko akutana na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 20 Novemba 2015 amekutana na kuzungumza na Rais Petro Poroshenko wa Ukraine ambaye baadaye amekutana pia na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Viongozi hawa wawili katika mazungumzo yao, wameridhishwa na uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican na Ukraine. Lakini sehemu kubwa ya mazungumzo yao yamejikita katika vita na kinzani za kijamii zinazoendelea kufuka moshi nchini Ukraine. Ni matumaini ya viongozi hawa wawili kwmaba, wadau mbali mbali wanaohusika wataweza kutekeleza wajibu wao kadiri ya Mkataba wa Minsk. Wamesikitishwa na hali ngumu ya maisha ambayo wananchi wengi wa Ukraine wanakabiliana nayo kwa sasa.

Baba Mtakatifu na mwenyeji wake wanatumaini kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kupeleka watu wenye uzoefu na kinzani za kijamii ili kusaidia mchakato wa kupata suluhu ya kudumu. Ukraine inahitaji kwa sasa huduma ya afya pamoja na kubadilishana mateka wa vita, kwani hali ngumu ya uchumi inaendelea kutisa maisha ya wananchi wengi wa Ukraine. Mkutano wa Baba Mtakatifu pamoja na Rais wa Ukraine imekuwa ni fursa makini ya kuweza kujadili pia mchango wa Kanisa katika jamii ya Ukraine bila kusahau mchango unaotolewa na Kanisa la Kigriki la Kikatoliki nchini humo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.