2015-11-20 11:18:00

Rais Kenyatta anamsihi Rais Nkurunziza kuanza tena mchakato wa majadiliano


Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kuishinikiza Serikali ya Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi kuanza mchakato wa majadiliano ya vyama vya upinzani, ili kuiepusha Burundi kutumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo itasababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Hivi karibuni, China pamoja na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya wamemshauri Rais Nkurunziza kuanza mchakato wa majadiliano kwa ajili ya ustawi, amani na maendeleo ya wananchi wa Burundi.

Tangu mwezi Aprili 2015  na hatimaye uchaguzi mkuu uliohitimishwa hivi karibuni kumekuwepo na machafuko ya kisiasa kwa vyama vya upinzani kumpinga Rais Nkurunziza kwa kujitwalia madaraka kinyume cha Katiba ya nchi na Mkataba wa Arusha wa mwaka 2000 uliohitimisha vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi iliyokuwa imedumu kwa takribani miaka kumi na miwili. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi sasa kuna idadi kubwa ya wananchi wasiokuwa na hatia wameuwawa kikatili na kwamba, zaidi ya wananchi 217, 000 wamekimbia Burundi ili kutafuta hifadhi ya maisha yao katika nchi jirani.

Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa ina wasi wasi wa kuzuka kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe hali ambayo itakuwa ni hatari sana kwa mafungamano ya kijamii nchini Burundi, kwa kukumbuka mauaji ya kimbari yaliyojitokeza nchini Rwanda kunako mwaka 1994. Hofu hii ndiyo ambayo inaendelea kuwasukuma viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kumtaka Rais Nkurunziza kufanya majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi na vyama vya upinzani ili hatimaye amani na utulivu viweze kurejea tena nchini Burundi.

China kwa upande wake inasema, ingependa kuona amani na utulivu vikirejea tena nchini Burundi ili kukuza mchakato wa uchumi na maendeleo ya watu. China pamoja na Jumuiya ya Kimataifa wako tayari kutoa msaada utakaoiwezesha Burundi kurejea tena kwenye majadiliano yanayopania kuleta amani na utulivu miongoni mwa wananchi ambao kwa sasa wanaishi kwa hofu kubwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.