2015-11-20 13:50:00

Mapadre wanahistoria na tamaduni zao! Ni wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa


Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Tamko kuhusu Seminari, “Optatam totius” na Tamko juu ya Mapadre “Presbyterorum ordinis” , hizi ni nyaraka muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Ni nyaraka ambazo zinajikita katika malezi na majiundo awali na endelevu ya Wakleri yanayojenga uzoefu fungamanishi kwa ajili ya ufuasi wa Kristo.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, kunako mwaka 2013 akafanya maboresho kwa kurejesha Seminari chini ya Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri. Baraza hili likapewa dhamana ya kuhakikisha kwamba, Wakleri wanakuwa na majiundo awali na endelevu katika maisha na utume wa Kanisa. Lengo ni kuhakikisha kwamba, miito inakuzwa na kupaliliwa, ili kuweza kuzalisha Wakleri watakatifu kwa kutambua kwamba, utakatifu wa maisha ya Padre unaanza seminarini!

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 20 Novemba 2015 wakati alipokuwa anazungumza na wajumbe wa kongamano la maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu kuchapishwa kwa nyaraka za Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Seminari na Maisha ya Mapadre, kwa kutambua kwamba, Mapadre ni viongozi walioteuliwa miongoni mwa waamini kwa ajili ya waamini kwa mambo yanayomhusu Mungu. Wanayo dhamana ya kutoa sadaka na kuwaondolea watu dhambi zao na kwamba, wanaishi kati ya watu kwa ajili ya watu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mapadre ni watu wanaozaliwa katika mazingira ya kibinadamu, kumbe wanapaswa kufumbatwa na tasaufi ya watu ili kukuza na kudumisha mahusiano mema. Mapadre ni watu wenye historia wanayopaswa kuikuza na kuidumisha katika mchakato mzima wa malezi na majiundo yao. Historia hii imwilishwe katika wito wa kuwa ni mfuasi wa Kristo katika huduma ya Kipadre inayopaswa kushuhudiwa katika maisha kwa kutambua kwamba, familia ni kiini cha wito na maisha ya kipadre.

Wahamasishaji wa shughuli za miito ndani ya Kanisa wanapaswa kukumbuka umuhimu wa familia kwani hapa wanakutana na Kanisa dogo la nyumbani, mahali pa majindo makini kiutu na chachu ya kiu ya wito na maisha ya Kipadre, tayari kuanza kujisadaka na kuonesha moyo wa ukarimu. Familia inaweza kupata mwelekeo mpana zaidi kwa kujumuisha: Shule, Parokia, Vyama vya kitume na makundi ya marafiki. Hapa ni mahali ambapo Wakleri wanajifunza kuishi kwa pamoja ili kukuza maahusiano ya kijamii.

Baba Mtakatifu anasema Padre mwema kwanza kabisa ni mtu mwema pia anayeifahamu historia ya maisha yake; anatambua utajiri  na mapungufu yake ya kibinadamu, tayari kujirekebisha ili kuwa na maisha bora zaidi, kwa kujikita katika utulivu wa ndani kielelezo makini cha mfuasi wa Kristo. Majiundo makini ni muhimu sana kwa Wakleri ili kujifunza kutumia vyema karama na mapaji yao badala ya kuelemewa na mapungufu yao ya kibinadamu. Padre ni mtu wa amani anayepaswa kusambaza amani hata wakati wa shida na magumu, ili kuwashirikisha wengine mahusiano mema na Mwenyezi Mungu. Haipendezi kumwona Padre anayesikitika, mwenye moyo mgumu na aliyechanganyikiwa kwani hii ni hatari kwa Padre mwenyewe na kwa wale wote wanaomzunguka!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mapadre wanapaswa kuwa ni mitume wa furaha na watangazaji mahiri wa Habari Njema ya Wokovu na kwamba, zawadi ya maisha na wito wa Kipadre inahifadhiwa katika chombo cha udongo, kinachopaswa kutunzwa kwa uangalifu mkubwa, ili kuwashirikisha wengine uzuri wa zawadi ya Upadre. Padre ana mizizi na utamaduni wake na ameitwa kutoka kati ya watu kwa ajili ya watu kwa mambo matakatifu na kwa ajili ya huduma kwa ndugu zake katika Kristo. Padre ni kielelezo cha Kuhani mkuu, Mhudumu na Mchungaji mwema anayepaswa kuwachunga watu wake kwa moyo mkuu!

Mapadre wanatumwa kuwahudumia watu ili waweze kuonja huruma ya Mungu katika maisha yao kwa njia ya Neno, lakini zaidi kwa ushuhuda wa maisha. Mapadre wamepakwa mafuta kwa ajili ya huduma na wala si kwa ajili ya kujitafuta wao wenyewe! Ni wahudumu wa Familia ya Mungu na Jamii katika ujumla wake na ndiyo maana wanapaswa kufundwa barabara ili waweze kutekeleza dhamana hii kwa moyo mkuu.

Mapadre wafundwe katika maisha ya kiroho, kiutu na kiakili ili kuwajengea ari na moyo wa kimissionari, tayari kutekeleza dhamana waliyokabidhiwa na Kristo Yesu kwa njia ya Kanisa. Mapadre wakumbuke kwamba, daima wako kati ya watu kwa ajili ya watu, daima wakijitahidi kuwahudumia kwa moyo wa unyenyekevu, ili kuwaonjesha uzuri unaofumbatwa katika Injili na upendo wa Mungu unaoshuhudiwa kwa njia ya wito na maisha ya Kipadre.

Baba Mtakatifu anawauliza Mapadre leo hii wameweka wapi hazina yao? Je, wako tayari kumjibu na kumwonesha Kristo Yesu mahali walipoihifadhi? Je, iko kati ya watu anaoishi na kusali nao; anaoshirikiana nao katika shifa, raha na majonzi ya maisha? Au hazina yake ameihifadhi katika malimwengu? Ni wakati wa kutafuta hazina ya maisha na wito wa Kipadre, tayari kutekeleza dhamana na wito wa Kipadre ambao Mama Kanisa amewakabidhi watoto wake. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, kongamano hili litaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa kwa wakati muafaka, ili kuwapata Mapadre wema na watakatifu kadiri ya matakwa ya Yesu Kristo mwenyewe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.