2015-11-20 15:28:00

Mafuruko ya salam na pongezi kwa Rais John Pombe Magufuli!


Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mheshimiwa Filipe Jacinto Nyusi amemtumia Salamu za Pongezi Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015. “Napenda kuchukua fursa hii kukuhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa niko tayari kufanya kazi nawe, ili kuimarisha uhusiano wa kirafiki na wa kihistoria uliopo na ushirikiano baina ya nchi zetu mbili”, amemueleza Rais Magufuli katika Salamu zake. Mheshimiwa Nyusi amesema Msumbiji na Tanzania zinaunganishwa na historia, utamaduni na kizazi kimoja, vitu ambavyo vinasaidia sana katika kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo, pamoja na majadiliano ambayo tumekuwa nayo katika masuala muhimu yanayohusu mahusiano yetu na maslahi yetu kimataifa. Katika Salamu zake hizo, Mheshimiwa Nyusi amemtakia afya njema Rais Magufuli, huku akiwatakia wananchi wa Tanzania maendeleo na ustawi. Vilevile amempongeza Mheshimiwa Rais kutokana na Uchaguzi Mkuu uliofanyika kuendeshwa kwa uhuru, haki, utulivu na uwazi.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam, Mheshimiwa Truong Tan Sang amemtumia Salamu za Pongezi Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais Sang amesema ana matumaini makubwa kwamba chini ya uongozi wa Mheshimiwa Magufuli na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wananchi wa Tanzania watapata mafanikio makubwa zaidi katika ujenzi wa Taifa tajiri na lenye mafanikio. “Nategemea pia kwamba uhusiano wa kiutamaduni na kirafiki katika nyanja mbalimbali kati ya Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yatajengwa na kuimarishwa zaidi, hivyo kuchangia katika kuimarisha amani, msimamo na ustawi wa nchi hizi mbili za Vietnam na Tanzania,” amesema Rais Sang. Aidha katika Salamu zake, Rais huyo wa Vietnam amemtakia kila la heri na afya njema Mheshimiwa Magufuli, na kumhakikishia ushirikiano wake mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yake.

Naye Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Dkt. Stergomena Lawrence Tax amemtumia Salamu za Pongezi Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Katika Salamu zake za Pongezi, Dkt. Stergomena Tax amesema ameupokea ushindi huo wa Mheshimiwa Magufuli kwa furaha na matumaini makubwa, na kwamba ushindi huo unadhihirisha matumaini na imani kubwa waliyo nayo kwake Watanzania. Vilevile amesema Jumuiya za Kikanda ikiwa ni pamoja na SADC, zina imaini kubwa na uwezo wa Mheshimiwa Magufuli ambao umejidhihirisha katika kusimamia masualambalimbali katika nyadhfa tofauti alizowahi kuzishika ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa sera na sheria za nchi, na mipango ya kuleta maendeleo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. “Watanzania na SADC tumepata kiongozi bora ambaye atatekeleza kwa vitendo shughuli za kuleta maendeleo na kuimarisha utawala bora na uwajibikaji”, ameongeza kusema Dkt. Stergomena.

Aidha Dkt. Stergomena ametumia nafasi hiyo ya Salamu zake kumkaribisha rasmi Rais Magufuli kama Mjumbe wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali (Summit) wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na hususan kama Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya SADC ya Ulinzi na Usalama(Organ). Amemuahidi Mheshimiwa Rais kumpatia taarifa muhimu kwa wakati ambao Mheshimiwa Rais atampangia. Dkt. Stergomena amemalizia Salamu zake kwa kumwombea heri Mheshimiwa Rais na Serikali atakayoiunda, na kuahidi kwamba yeye binafsi pamoja na Jumuiya ya SADC watatoa ushirikiano wa dhati kwa Mheshimiwa Rais; Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Serikali nzima ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakati huo huo, Rais Jamhuri ya Botswana, Mheshimiwa Luteni Jenerali Seretse Khama Ian Khama, amemtumia Salamu za Pongezi Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. “Kuchaguliwa kwako ni uthibitisho wa imani waliyo nayo wananchi wa Tanzania katika uwezo ulio nao wa kutoa msukumo kwa nchi yako kufikia hatua za juu zaidi katika suala zima la maendeleo ya kijamii na kiuchumi”, amesema Rais Khama katika Salamu zake. Rais Khama amemueleza Rais Magufuli kuwa wakati huu anapochukua majukumu makubwa ya Urais, anamhakikishia kwamba yuko tayari kuendeleza mahusiano ya kirafiki na ushirikiano wa nchi mbili za Botswana na Tanzania pamoja na watu wake. “Nina imani kwamba chini ya uongozi wako, ushirikiano mzuri na wa karibu ambao nchi zetu mbili zimekuwa nao utaendelea kukua na kuwa imara zaidi”, ameongeza kusema Rais Khama katika Salamu zake. Katika Salamu zake hizo, Rais Khama memtakia Rais Magufuli mafanikio na afya njema.

Habari zaidi zinasema Rais wa Ireland, Mheshimiwa Michael D. Higgins amemtumia Salamu za pongezi Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika Salamu zake hizo, Rais Higgins amesema Ireland na Tanzania zimekuwa na uhusiano mzuri na wa kirafiki kwa miaka mingi, hivyo ana matarajio kwamba katika kipindi cha uongozi wa Rais Magufuli, uhusiano huo utaimarishwa zaidi. “Ireland na Tanzania zimekuwa na mipango ya maendeleo na ushirikiano kwa miaka mingi katika nyanja za kilimo na lishe, uimarishaji wa huduma za afya na uendelezaji wa utawala bora na uwajibikaji”, amesema Rais Higgins katika Salamu zake. Aidha, amesema Ireland inavutiwa na maendeleo ya kiuchumi na kijamii yaliyokwisha kufanywa na Tanzania katika miaka ya karibuni, hivyo nchi hiyo itaendeleza ushirikiano wake na Mheshimiwa Magufuli na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naye Rais wa Jamhuri ya Ghana, Mheshimiwa John Dramani Mahama amemtumia Salamu za Pongezi Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akisema kuwa kuchaguliwa kwake kunaonyesha imani waliyo nayo wananchi wa Tanzania katika uongozi na maono yake kwa taifa. “Nina matarajio makubwa ya kushirikiana nawe katika kuimarisha uhusiano wa karibu na wa kirafiki uliopo kati ya Tanzania na Ghana kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili”, ameongeza kusema Rais Mahama. Rais huyo wa Ghana amesema ana imani kuwa nchi hizi mbili zitatafuta fursa zaidi siyo tu katika kiwango cha ushirikiano wa kirafiki bali katika maeneo mengi, ili kupata maendeleo zaidi na pia kujihakikishia amani na usalama katika Afrika na duniani kwa ujumla. Aidha Rais Mahama amemtakia afya njema Rais Magufuli katika utekelezaji wa majukumu yake

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mheshimiwa Robert Gabriel Mugabe amemtumia Salamu za Pongezi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015. Mheshimiwa Mugabe amesema kuchaguliwa kwa Mheshimiwa Magufuli kushika wadhifa huo mkubwa wa kuongoza nchi, ni kielelezo cha imani kubwa waliyo nayo kwake wananchi wa Tanzania na kwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM). “Unapoanza majukumu yako ya Urais, napenda kukuhakikishia ushirikiano wa dhati kutoka Serikali yangu. Wananchi wa Zimbabwe wataendeleza mahusiano ya kihistoria, kisiasa na kiutamaduni yaliyopo kati ya nchi zetu mbili, na ushirikiano tulioujenga wakati wa mapambano dhidi ya ukoloni”,ameendelea kusema Rais Mugabe katika Salamu zake. Aidha, Rais Robert Mugabe amemhakikishia Rais Magufuli kuwa atafanya naye kazi kwa karibu ili kuendeleza uchumi wa wananchi wa nchi hizi mbili, huku akimtakia mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yake.

Na mwandishi maalum kutoka Dar es Salaam.








All the contents on this site are copyrighted ©.